IQNA

Msikiti wateketea kwa moto Michigan, Marekani

17:48 - March 13, 2017
Habari ID: 3470893
IQNA-Moto umeteketeza Msikiti na Kituo Kiislamu cha Ypsilanti mjini Pittsfield, jimboni Michigan nchini Markeani

Taarifa zinasema kuwa, moto huo ulizuka Jumamosi saa 11 Alasiri na kuteteteza kituo hicho ambacho hutumika pia kama msikiti lakini hakuna mtu aliyepoteza maisha au kujeruhiwa katika tukio hilo. Jengo hilo limeharibiwa kabisa na moto huo na haliwezi kukarabatiwa.

Walioshuhudia wanasema moto uliteketea haraka sana na kuliharibu jengo kabla ya wazimamoto kuwasilia.

Hadi sasa haijabainika chanzo cha moto huo huku baadhi wakisema yamkini ni kitendo cha jinai kilichotekelezwa na watu wenye chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu (Islamophobes).

Dawud Walid, Mkurugenzi wa tawi la Michigan la Baraza la Uhusiano wa Uislamu na Marekani (CAIR) ametoa taarifa na kutaka maafisa wa usalama wachunguze kikamilifu chanzo cha moto huo.

"Tunatoa wito kwa maafisa wa serikali kutumia uwezo wao wote kuchunguza moto huu na iwapo itabainika ni kitendo cha jinai, wachunguze sababu zake," alisema Walid.

CAIR imesema ikibainika kuwa ni kitendo cha jinai, itatoa zawadi ya $1,000 kwa yeyote atakayetoa habari zitakazopelekea kukamatwa mhusika au wahusika.

Walid anasema kuna uwezekano kuwa moto huo ni wa makusudi kwani baadhi ya wakaazi wamewahi kupinga ujenzi wa shule ya Kiislamu mjini humo. Mwaka 2011, pendelezo la kujenga shule lilipingwa na manispaa ya mji huo. Baada ya Waislamu kupeleka kesi mahakamani, walilipwa fidia ya $1.7 milioni.

Baada ya ushindi wa Trump na kuapishwa kwake Januari 20 kumeshuhudiwa hujuma dhidi ya misikiti na vituo vya Kiislamu Marekani na pia katika nchi jirani ya Canada.

Mwezi moja baada ya ushindi wa Trump katika uchaguzi wa rais Marekani mnamo Novemba 8 mwaka jana, Shirika la Southern Povert Law Centre (SPLC) lilirekedo vitendo 1,098 vya chuki kote Marekani ambapo idadi kubwa ya waliotekeleza vitendo hivyo walimtaja Trump na nara yake ya Kuifanya Marekani Kuwa na Nguvu Tena (Make America Great Again) au matamshi yake dhidi ya wanawake.

3462405

captcha