IQNA

Sarafu muhimu za Kiislamu katika maonyesho nchini Qatar

20:27 - March 14, 2017
Habari ID: 3470894
IQNA-Jumba la Makumbusho la Qatar ambalo lina mkusanyiko mkubwa zaidi za sarafu za Kiislamu duniani limeandaa maonyesho yenye sarafu muhimu zaidi ya Kiislamu duniani.

Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA, sarafu hizo zinaonyeshwa kwa mara ya kwanza katika maonyesho yaliyopewa jina la ‘Kazibora za Sarafu za Kiislamu’ ambayo yalifunguliwa Jumamosi katika Jengo la Makumusho ya Sanaa za Kiislamu (MIA) mjini Doha. Msomi wa elimu ya sarafu ambaye ni maarufu duniani Dkt. Alain Baron na ambaye anasimamia maonyesho hayo amesema, "Qatar ina mkusanyiko mkubwa zaidi wa sarafu za Kiislamu duniani na hadi leo ni wachache waliokuwa wakijua kuwepo mkusanyiko huu.”

Kwa muda wa miaka 40 sasa, serikali ya Qatar imekuwa ikikusanya na kununua sarafu za kale na hivi sasa ina mkusanyiko wa sarafu 100,000 za Kiislamu na aghalabu ni nadra sana na zimeonyeshwa kwa mara ya kwanza katika historia ya zama hizi anasema Dkt. Baron.

Katika maonyesho hayo kuna sarafu sita za dhahabu za Kiislamu ambazo ni kielelezo cha kuibua utambulisho wa Kiarabu na kustawi ulimwengu wa Kiislamu. Sarafu hizo zinasemekana kutumika katika karne ya Mtume Muhammad SAW na zina tarehe za zama zilizotumika pamoja na aya za Qur’ani.

Sarafu ya kwanza halisi ya ulimwengu wa Kiislamu inaaminika kuundwa katika zama za utawala wa Bani Ummaya wakati wa utawala wa Abd Al Malik bin Marwan mwaka 77 Hijria Qamaria (696 Miladia-CE). Huu ndio wakati ambao sarafu ya dinar ilianza kutumika na hadi sasa inatumika katika nchi nyingi za Kiarabu.

h3583728

captcha