Ilikuwa ni miaka 23 kabla ya Hijra ya Bwana Mtume Muhammad (rehema
za Allah ziwe juu yake na Aal zake) kutoka Makka kwenda Madina na ilikuwa ni
mwaka wa thelathini tangu mwaka wa ndovu, anga ya ardhi ya Makka katika usiku
wa siku hiyo iling'ara kwa nyota zilizotandawaa mbinguni. Nuru ya mbalamwezi
iliifanya Nyumba Tukufu ya Allah ya al Kaaba iwe na sura na mandhari ya aina
yake. Lahadha yoyote ile baada ya wakati huo alitarajiwa kuwasili mgeni wa
Mwenyezi Mungu na hujja Wake katika ardhi. Maumbo yote ya mbinguni na angani
yaliweka ahadi kuwa yataifanya kesho ya siku hiyo kuwa siku adhimu katika
kumbukumbu ya historia. Jua lilipochomoza, siku ya Ijumaa ya tarehe 13 Rajab,
ambayo ndiyo siku iliyoahidiwa, iliwadia.
Watu wote walimwona Fatima bint Asad wakati alipoizuru Nyumba ya Allah ya al
Kaaba jinsi alivyokuwa akinong'ona na Mola wake kwa kusema:" Ee Mola
wangu, mimi nimekuamini Wewe, na nimeyaamini yale yaliyokuja kutoka kwako,
kupitia Mitume wako na Vitabu vyako; na ninasadikisha maneno ya babu yangu
Ibrahim, na ni yeye ndiye aliyeijenga nyumba hii ya kale. Ninakuomba kwa jaha
ya yule aliyeijenga nyumba hii, na kwa jaha ya kizazi hiki kilichomo tumboni
mwangu, uniwezeshe kujifungua kwa wepesi." Kufumba na kufumbua na kwa
namna ya kimuujiza, Fatima bint Asad aliingia ndani ya al Kaaba; watu wote
walishangaa na kupigwa na butwaa. Na naam, katika lahadha hiyo alifumbua jicho
na kuja duniani Ali bin Abi Talib, mzaliwa wa fakhari na adhama wa al Kaaba,
chemchemu ya haki na uadilifu na johari na mfunguzi wa silsili ya Maimam
thenashara walioahidiwa.
Mtume SAW alisema "…Ali ni ndugu, wasii na khalifa wangu kwenu"
Wakati Imam Ali AS alipozaliwa, umri wa Bwana Mtume (rehema za Allah ziwe juu
yake na Aal zake) haukuwa umepindukia zaidi ya miaka thelathini. Miaka michache
baadaye, Mtukufu huyo alitoa shauri kwa Ami yake Abu Talib la kumsaidia ulezi
wa Ali kutokana na aila na familia kubwa aliyokuwa nayo ami yake huyo ili
kumpunguzia mzigo mzito wa gharama za kukidhi mahitaji ya familia yake. Abu
Talib aliafiki ushauri huo, na kuanzia kipindi cha utotoni mwake, Ali AS akawa
pamoja na Bwana Mtume katika kipindi chote cha umri wake. Ali alikuwa mtu wa
kwanza kumwamini Bwana Mtume. Alikuwa mpwekeshaji wa Allah tangu udogoni mwake
na hakuwahi hata mara moja kuabudu masanamu kama walivyokuwa watu wengi wa zama
hizo.
Baada ya Mtume Muhammad SAW kubaathiwa na kupewa Utume, kwa muda wa miaka
mitatu alikuwa akiwatangazia watu dini kwa siri, na hakuwa akifanya hivyo ila
kwa wale ambao alihisi kuna uwezekano wa wao kuukubali mwito wa Uislamu.
Alifanya hivyo kwa amri ya Mwenyezi Mungu aliposema: "Na uwaonye jamaa
zako walio karibu nawe." Baada ya kupita miaka mitatu, Malaika wa Wahyi
Jibril AS alishuka, na kwa amri ya Mola akamfikishia Bwana Mtume ujumbe wa
kumtaka aitangaze dini hadharani na kuanzia kwa jamaa na watu wake wa karibu.
Bwana Mtume SAW alitekeleza amri hiyo ya Allah kwa kuwaalika shakhsia na watu wakubwa
wakubwa wa ukoo wake wa Bani Hashim na akaanza kwa kuwaambia: "Hakuna mtu
yeyote duniani aliyewaletea watu wake kitu bora kama kile nilichokuleteeni
mimi. Mimi nimekuleteeni kheri yenu ya dunia na Akhera. Mola wangu ameniamuru
nikulinganieni Tauhidi na kukufikishieni wito wake wa kumwabudu Yeye Mola
Mpweke. Nani kati yenu atakayenisaidia katika jambo hili ili awe ndugu yangu,
wasii wangu na mwakilishi wangu kwenu?"
Katika lahadha hiyo kimya kizito kilitanda katika anga ya majlisi hiyo na watu
wote wakawa wameinamisha vichwa vyao chini wakiwa wamezama kwenye mawazo na
tafakuri. Ghafla Ali AS alivunja kimya hicho, akainuka na kumuelekea Bwana
Mtume na kumwambia:" Yaa Rasulallah, mimi nitakusaidia katika jambo
hili". Hapo Bwana Mtume akamtaka Ali akae kitako, na kwa mara nyengine
akarudia tena maneno yake. Alifanya hivyo mara tatu pasina kupata jibu lolote
kutoka kwa watu, na hivyo mara ya mwisho aliuweka mkono wake juu ya mkono wa
Ali na kusema:" Enyi watu wangu na jamaa zangu! Ali ni ndugu, wasii na
khalifa wangu kwenu". Na kwa njia hiyo wasii wa kwanza wa Bwana Mtume
akaainishwa na kutangazwa na yeye mwenyewe Mtume wa mwisho wa Allah.
Katika siku hiyo moja Bwana Mtume SAW aliutangaza Utume wake na Uimamu wa Ali
AS. Na kwa njia hiyo akawa amewatambulisha watu wote kuwa daraja mbili hizo
hazitenganiki, na Uimamu, ni mkamilishaji wa risala ya Utume.
Qur'ani Tukufu imezungumzo kujitolea muhanga Imam Ali AS
Katika mwaka wa 13 tangu alipobaathiwa Nabii Muhammad SAW, wakati
watu wa Yathrib yaani Madina walipombai Mtukufu huyo na kuahidi kumlinda na
kumhami, wakubwa wa Makureishi walihisi hatari inawakabili, hivyo wakaamua
kukutana na kufikiria la kufanya. Baada ya majadiliano marefu waliafikiana
katika kikao chao hicho kuwa wamuue Bwana Mtume. Lakini kumuua Bwana Mtume
halikuwa jambo rahisi, kwani kufanya hivyo kungezusha vita na kuwafanya Bani
Hashim watake kulipiza kisasi cha damu ya mtu wao. Kwa sababu hiyo wakaamua
kwamba kila kabila la Kikureishi litoe kijana mmoja, kisha vijana hao kwa
pamoja waende nyumbani kwa Bwana Mtume wakati wa usiku na kumshambulia kitandani
alipolala kwa kumkatakata kwa panga zao. Kwa kufanya hivyo Bani Hashim
hawatokuwa na uwezo wa kukabiliana na makabila yote, na kwa hivyo watalazimika
kukubali fidia tu ya damu ya mtu wao iliyomwagwa, na suala litaishia hapo.
Lakini Makureishi waliyapanga hayo bila kuwa na habari kwamba Mwenyezi Mungu
Mtukufu alishampa Mtume wake habari ya njama yao hiyo ovu na kumuamuru ahame
Makka na kuhajiri Madina. Pamoja na hayo ili kuizima njama hiyo ya Makureishi
kwa kuwababaisha wasiweze kung'amua habari ya Hijra ya Bwana Mtume, alihitajika
mtu wa kujitolea mhanga nafsi yake, ambaye angelala kwenye kitanda cha Mtukufu
huyo katika usiku huo, ili pale kundi la vijana wa Kikureishi litakapotaka
kuivamia nyumba ya Bwana Mtume lidhani kwamba yeye bado hajaondoka nyumbani
kwake na kwa njia hiyo Hijra ya Mtukufu huyo kuelekea Madina ifanyike bila
kizuizi. Mtu huyo wa kuwa tayari kujitolea mhanga roho yake hakuwa mwengine
ghairi ya Ali AS.
Wakati kundi la vijana wa Kikureishi liliposhikilia panga mikononi mwao na kuvamia
nyumba ya Mtume wa Allah, baina ya Ali na mauti ya kuuawa shahidi, yalikuwa ni
masafa ya pua na mdomo tu, lakini ghafla wauaji hao wakatanabahi kuwa ni Ali
ndiye aliyekuwa amelala kitandani pa Mtume. Qur'ani Tukufu imekuzungumzia
kujitolea mhanga huko kwa Ali AS katika aya ya 207 ya Suratul Baqaraha kwa
kusema: Na katika watu yupo ambaye huiuza nafsi yake kwa kutaka radhi za
Mwenyezi Mungu; na Mwenyezi Mungu ni Mpole kwa waja wake.
Ushujaa mkubwa wa Imam Ali AS
Maisha ya Ali bin Abi Talib AS tokea kipindi cha Hijra ya Bwana Mtume SAW hadi kuaga dunia mtukufu huyo yalitawaliwa na matukio mengi mno hususan yale yaliyoakisi moyo mkubwa wa kujitolea kwake mhanga katika medani za vita vya Jihadi. Baada ya ushindi wa Waislamu katika vita vya Badr, Makureishi walikuwa wameemewa na kufadhaika mno kutokana na taathira ya kushindwa katika vita hivyo, na kwa hivyo waliamua kujiandaa kwa jeshi kubwa na kujizatiti kwa zana na silaha chungu nzima katika vita vilivyofuatia vya Uhud, ili kulipiza kisasi cha kushindwa vibaya katika vita vya Badr na kisasi cha watu wao waliouawa katika vita hivyo. Awali, hata katika vita hivyo vya Uhud pia Makureishi walikuwa wameshashindwa, lakini wakati Waislamu walipokuwa wameshughulika kukusanya ngawira, wapiganaji wa Kiislamu waliopewa jukumu la kulinda ngome katika sehemu ya juu ya mlima Uhud na ambao walisisitizwa mno na Bwana Mtume wasije wakaondoka mahala hapo katika hali yoyote ile kwa kuona wenzao wameshinda au wanashindwa, walighafilika na agizo hilo la Mtume na badala yake wakakimbilia kwenye ngawira.
Wakati huo, Khalid ibn Walid mmoja wa makamanda wa jeshi la makafiri
wa Kikureish aliyekuwa akivizia na kungojea fursa kama hiyo aliliongoza jeshi
la wapanda farasi kupitia kwenye ngome iliyoachwa tupu na wapiganaji wa jeshi
la Waislamu na kuanza kuwashambulia Waislamu kutokea nyuma. Katika hali hiyo ya
tafrani na hamkani maadui wakaeneza uvumi pia kwamba Bwana Mtume ameuawa.
Waislamu wengi walirudi nyuma, wakatawanyika na kusambaratika ukiachia wachache
walioendelea kubaki pamoja na Mtume wa Allah. Ni katika lahadha hiyo ndipo
ilipoonekana kwa uwazi kabisa nafasi na mchango mkubwa wa Ali AS.
Kwa ushujaa usio na mfano Ali alipambana kwa upanga wake bega kwa bega na Bwana
Mtume huku akimlinda Mtukufu huyo kutokea kila upande mbele ya mashambalio ya
mtawalia ya washirikina. Ibn Athir, mwanahistoria, mwanafasihi na mpokezi
maarufu wa hadithi, ameandika katika kitabu chake kiitwacho 'al Kaamil fit
Taarikh' kwamba: "Mtume SAW aliliona kundi la washirikina waliokuwa
wameazimia kufanya shambulio; akamuamuru Ali awashambulie. Kwa amri ya Mtume,
Ali aliwashambulia washirikina hao, na kutokana na kuwaua kadhaa miongoni mwao
walitawanyika na kusambaratika. Kisha mara Mtume akaliona kundi jengine, na
hapo akamuamuru Ali alishambulie, na Ali akalishambulia na kuwaua na kuwasambaratisha.
Katika lahadha hiyo Malaika wa Wahyi alimuelekea Bwana Mtume na kumwambia:
"Huu ulioonyeshwa na Ali, ni upeo wa juu kabisa wa kujitolea mhanga".
Naye Bwana Mtume akajibu kwa kusema:" Yeye anatokana na mimi, na mimi
ninatokana na yeye". Katika lahadha hiyo ikasikika sauti kutoka mbinguni
ikinadi:
لا فَتى اِلاّ عَلِىّ، لا سَیفَ اِلاّ ذُو الفَقار
"Hakuna shababi mithili ya Ali, wala hakuna upanga
mithili ya dhulfiqar"
Mbali na ushujaa huo mkubwa wa Imam Ali AS katika vita vya Uhud, ushujaa wake
ulionekana pia katika vita vyote alivyoshiriki mtukufu huyo. Imam Ali alikuwa
anajulikana pia kwa jina la 'Faatihu Khaybar', yaani mtu aliyewezesha
kupatikana ushindi na kukombolewa ngome ya Khaybar na kisa cha kukombolewa
ngome hiyo ya Khaybar ni maarufu.
Bila ya shaka kuna mengi mno ya kueleza na kusimulia kuhusiana na jinsi Imam
Ali AS alivyokuwa pamoja na bega kwa bega na Bwana Mtume, katika kipindi chote
cha maisha ya mtukufu huyo na mengi aliyoyafanya kujitolea kwa ajili ya Uislamu
3588749