IQNA

Polisi Mwanamke Mwislamu aliyekufa akiwalinda Wakristo aenziwa Misri

12:16 - April 13, 2017
Habari ID: 3470933
TEHRAN (IQNA)- Watu wa Misri wanamuenzi afisa wa polisi mwanamke Mwislamu ambaye alipoteza maisha yake akijijaribu kumzuia gaidi wa kundi la ISIS kuingia katika kanisa la Kikhufti (Coptic) mjini Alexandria.

Siku ya Jumapili kundi la kigaidi la ISIS lilitekeleza hujuma za mabomu dhidi ya makanisa mawili ya Kikhufti katika miji ya Tanta na Alexandria kaskazini mwa Misri na kuua Wakristo wasiopungua 47.

Hujuma ya kwanza ilipelekea watu 29 kuuawa na wengine zaidi ya 70 kujeruhiwa katika wa bomu dhidi ya Kanisa la Kikhufti katika mji wa Tanta, eneo la Nile Delta. Masaa kadhaa baada ya hujuma hiyo bomu jingine liliripuka nje ya kanisa la Mtakatifu Mark mjini Alexandria ambapo watu 18 waliuawa na wengine karibu 30 kujeruhiwa. Imearifiwa kuwa kiongozi wa Kanisa la Kikhufti Misri Papa Tawadros II alikuwa ameondoka katika kanisa hilo muda mfupi kabla ya mlipuko huo.

Afisa wa polisi Bi. Nagwa Abdel-Aleem aliyekuwa na umri wa 55 alikuwa analinda lango la kanisa hilo la mjini Alexandria wakati gaidi aliyekuwa amejifunga mshipi wa bomu alipojaribu kupita katika kituo cha upekuzi. Baada ya kuziwa na Bi. Abdel-Aleem kupita, gaidi huyo alijilipua katika mlango wa kanisa. Duru zinasema gaidi huyo alikuwa amelenga kumuua Papa Tawadros II.

Bi. Abdel-Aleem ni afisa wa kwanza wa polisi mwanamke kupoteza maisha akiwa kazini nchini Misri. Vyombo vya habari nchini humo vimeripoti kuwa, wanae wawili wa marehemu Bi. Abdel Aleem ni maafisa wa polisi na kwamba mmoja kati yao pia alipoteza maisha katika tukio hilo.

Picha Bi Nagwa akiwa na mume wake ambaye ni luteni katika jeshi la Misri imesembaa katika mitandao ya kijamii huku wengi wakimshukuru marehemu kwa kujitolea katika kazi yake.

Gazeti la Independent la Uingereza limeandika katika Twitter hivi: "Afisa wa polisi Mwislamu mwenye kuvaa Hijabu amepoteza maisha akilinda Kanisa Kuu la Kikhufti mjini Alexandria. Usiwahukumu watu kwa vazi lao, vitendo ndio kigezo."

Hujuma hiyo ilijiri wakati waumini wa Kikristo walikuwa wakiadhimisha siku ijulikanayo kama Jumapili ya Matawi ambayo huwa wiki moja kabla ya Pasaka.

Kuna Wakristo milioni 10 kati ya watu wote milioni 90 nchini Misri. Mara kwa mara Wakristo wa Misri hukabiliwa na hujuma za kundi la kigaidi la ISIS au waitifaki wao na hujuma hizo zimeongezeka baada ya mwamko wa 2011.

Kituo cha Kiislamu cha Al Azhar nchini Misri kimetoa taarifa na kulaani vikali hujuma hizo mbili za kigaidi dhidi ya makanisa nchini humo.

Inafaa kukumbusha hapa kuwa, magaidi wa ISIS sawa na wenzao wa Al Qaeda, Boko Haram na Al Shabab wanafuata itikadi yenye misimamo mikali ya Uwahhabi ambao ni itikadi inayotawala Saudia. Hii ni itakadi ambayo inapigiwa debe na watu wanaopata himaya ya Saudia ambao wanawavutia magaidi kote duniani. Magaidi wa ISIS wanatumia itikadi ya Uwahhabi kuwatuhumu Waislamu wengine kuwa ni makafiri na pia kuwalenga wasiokuwa Waislamu na hivyo kuwaua kiholela.


captcha