Baada ya shambulio la Wazayuni katika haram ya Nabii Ibrahim AS, eneo hilo liligawanywa sehemu mbili, lengo likiwa ni kuufanya utawala ghasibu uidhibiti sehemu kubwa ya haram hiyo kwa kuendeleza ukaliaji wake wa mabavu, kusababisha hali ngumu ya maisha kwa wananchi wa Palestina na kuweka kambi za Kizayuni kwa madhumuni ya kuidhibiti kikamilifu haram hiyo.
Aidha tangu msikiti mtukufu wa Al-Aqsa ulipochomwa moto hadi sasa, utawala haramu wa Israel umekuwa ukifanya kila njama ili kufanikisha ndoto yake ya kuubomoa kikamilifu msikiti huo mtukufu, ambapo hatua kwa hatua umekuwa ukitekeleza mipango ya kukiyahudisha kikamilifu kibla hicho cha kwanza cha Waislamu na kubadilisha muundo wake wa Kiislamu na Kiarabu. Uchimbaji mkubwa wa mashimo ya chini ya ardhi chini ya msikiti wa Al-Aqsa unaoendelea hadi sasa ni hatari kubwa inayotishia uwepo wa mahala hapo patakatifu. Wazayuni aidha wameuzingira msikiti huo kwa kujenga masinagogi yapatayo 100 pamoja na vituo vingine vya kiyahudi.
Kitendo cha Israel cha kufuta athari yoyote ile ya Kiislamu na kihistoria ya taifa la Palestina na kubadilisha muundo wa kijiografia na wa idadi ya watu kandokando ya maeneo hayo inalenga kupachika badala yake alama na nembo bandia katika ardhi ya Wapalestina. Utawala wa Kizayuni umekuwa ukitekeleza kila mara sera ya kuyapa sura ya Kizayuni maeneo ya ardhi za Palestina kwa kupotosha ukweli wa mambo kwa njia ya kubomoa turathi za Kiislamu, nyumba na majengo ya kihistoria ya Wapalestina na kujenga badala yake mahekalu ya kiyahudi.
UN yauonya utawala wa Israel
Hii ni katika hali ambayo, maazimio nambari 242 na 338 ya Umoja wa Mataifa pamoja na mkataba wa nne wa Geneva yameuonya utawala wa Kizayuni kwa kuutaka ujiepushe na kuyatwaa na kuyatumia kwa namna yoyote ile maeneo ya ardhi za Palestina unayoyakalia kwa mabavu. Jinai za utawala habithi wa Israel za kubomoa na kuyavunjia heshima maeneo na majengo ya Kiislamu na kuyadhibiti maeneo hayo kwa lengo la kuwafukuza Wapalestina wote katika mji mtakatifu wa Baitul Muqaddas na maeneo mengine ya Palestina vinadhihirisha sera za kibaguzi za utawala huo ghasibu za kukabili na uhuru wa kuabudu wa wafuasi wa dini hizo za mbinguni, na na dini za Mwenyezi Mungu.