IQNA

Polisi Nigeria wahujumu maandamano ya amani ya Waislamu

16:17 - April 18, 2017
Habari ID: 3470939
TEHRAN (IQNA)-Polisi nchini Nigeria kwa mara nyingine tena wamtumia gesi ya kutoa machozi kuhujumu maandamano ya amani ya Waislamu katika mjimkuu Abuja.

Taarifa zinasema Waislamu hao wameandamana kwa njia ya amani ili kuishinikiza serikali kutekeleza amri ya mahakama ya kumwachilia huru Sheikh Ibrahim Zakzaky, kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria, hata hivyo polisi wa nchi hiyo wametumia mabomu ya kutoa machozi na maji ya sumu kuwatawanya mamia ya Waislamu hao.

Wengi wa Waislamu hao walikuwa ni wanawake na waliitisha maandamano hayo Jumatatu ili kuishinikiza serikali imwachilie huru Sheikh Zakzaky ambaye anaendelea kushikiliwa na serikali licha ya Mahakama Kuu ya Nigeria kutoa amri ya kuachiliwa huru.

Itakumbukwa kuwa Sheikh Ibrahim Zakzaky akiwa na mke wake walitekwa nyara na Jeshi la Nigeria mwezi Disemba mwaka 2015 katika kituo cha kidini huko katika mji wa Zaria jimboni Kaduna. Tokea wakati huo Sheikh Zakzaky na mkewe wamekuwa wakizuiliwa katika mojawapo ya vituo vya kijeshi vya nchi hiyo bila kufunguliwa mashktaka.

Hivi karibuni Harakati ya Kiislamu Nigeria (INM) ilitahadharisha kuwa kiongozi wa harakati hiyo, Sheikh Ibrahim Zakzaky huenda akapoteza uwezo wa kuona na kuwa kipofu akiwa kizuizini.

Jeshi hilo lilidai kuwa wafuasi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria walikuwa na njama ya kutaka kumuua Mkuu wa Jeshi la Nigeria, madai ambayo yamekanushwa vikali na wafuasi wa harakati hiyo.

Jeshi hilo katili liliizika miili ya waliouawa katika kaburi moja kwa lengo la kuficha ushahidi wa ukubwa wa jinai hiyo. Inakadiriwa kuwa Waislamu 1000 wasio na hatia waliuawa katika tukio hilo huku Sheikh Zakzaky, ambaye hali yake ya kiafya si nzuri, akiendelea kushikiliwa korokoroni pasina kufunguliwa mashtaka.

/3462615
captcha