IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Uadui wa Marekani dhidi ya Iran umekuwepo kwa sura tofauti

23:14 - April 19, 2017
Habari ID: 3470940
TEHRAN (IQNA)-Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, hakuna shaka yoyote kuhusu uadui wa madola ya kibeberu hususan Marekani dhidi ya taifa la Iran na kwamba uadui huo umekuwa ukioneshwa muda wote kwa sura tofauti.

Ayatullah Ali Khamenei amesema hayo leo asubuhi mjini Tehran wakati alipoonana na makamanda na maafisa wa vikosi vya ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa mnasaba wa maadhimisho ya Siku ya Jeshi na kubainisha kuwa, nguvu na uwezo wa kusimama kidete taifa la Iran na kutoshughulishwa kwake na makeke na hamaki za Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya ni mambo ambayo yataendelea kuwepo. Aidha amesisitiza kuwa, wenye jukumu kubwa zaidi la kusimama kidete na kutomuogopa adui ni vikosi vya ulinzi, wanauchumi na watu wa masuala ya kiutamaduni, kielimu na kiutafiti.

Amesema, moja ya mambo yanayolifanya taifa la Iran kuwa imara sana ni moyo wake wa kishujaa na kusimama kwake kidete mbele ya makeke na upayukaji wa madola ya kibeberu.

Ameongeza kuwa, moja ya hila na ujanja unaotumiwa na madola ya kiistikbari ni kuyatisha mataifa na tawala za nchi nyingine na kutumia woga wa mataifa hayo kufanikisha malengo haramu ya madola hayo ya kibeberu na ndio maana mara zote utayaona madola hayo ya kiistikbari yanapenda kujigamba sana na kujionesha yana nguvu kubwa.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa, adui yeyote yule, awe Mmarekani au madola mengine ya kiistikbari, hawezi kufanya lolote mbele ya mfumo wa utawala unaotegemea vizuri nguvu za wananchi wake.

Vile vile amesema, hatua ya Imam Khomeini MA, mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ya kutangaza Siku ya Jeshi humu nchini ilikuwa ni ya hekima ya hali ya juu.

Vile vile Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria namna maadui wanavyofanya njama za kuvuruga uchaguzi ujao nchini Iran na kusema kwamba, taifa la Iran liko macho na litakabiliana vilivyo na njama hizo za maadui.

3591203/

captcha