IQNA

Mashindano ya Kimataifa ya Qur’ani ya Iran yafunguliwa rasmi

23:50 - April 19, 2017
Habari ID: 3470941
TEHRAN (IQNA)-Mashindano ya 34 ya Kimataifa ya Qur’ani Tukufu ya Iran yamefunguliwa rasmi Jumatano hii katika Ukumbi wa Sala wa Imam Khomeini MA mjini Tehran.

Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA, mashindano hayo yamefunugliwa katika sherehe iliyohudhuriwa na Ayatullah Mohammadi Golpaygani, mkuu wa Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ali Larijani Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu, Bunge la Iran, Hujjatul Islam Ali Mohammadi, Mkuu wa Shirika la Waqfu na Mambo ya Kheri Iran na maafisa wengine wa ngazi za juu katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wakiwemo wasomi na wataalamu wa Qur’ani Tukufu.

Sherehe hiyo ilianza kwa qiraa ya Qur’ani Tukufu ya Ustadh Sayyed Jawad Husseini, qarii wa kimataifa kutoka mji wa Mashhad kaskazini mashariki mwa Iran.

Ujumbe wa Rais Rouhani

Ujumbe wa Rais Hassan Rouhani wa Iran umesomwa katika sherehe za ufunguzi na Waziri wa Utamaduni na Muongozo wa Kiislamu Sayyed Ridha Salehi Amiri. Katika sehemu ya ujumbe wake, Rais Rouhani amesema Qur’ani Tukufu ni kitabu chenye lengo la kumuokoa mwanadamu na kumuondoa katika mkwambo. Rais wa Iran amesema mwanadamu wa leo anahitaji kuifahamu Qur’ani zaidi na kutekeleza mafundisho yake.

Mwanadamu anakamilika kwa kurejea katika Qur’ani

Akizungumza katika ufunguzi wa mashindano hayo ya kimataifa ya Qur’ani, Ali Larijani amesema mwanadamu ataweza kukamilika tu kwa kurejea katika mafundisho ya Qur’ani Tukufu kwani Mwenyezi Mungu amekiteremsha kitabu hicho kiwe muongozo hasa katika mazingra ya sasa magumu ya maisha ambayo Waislamu wanakabiliana nayo duniani.

Mashindano ya kipekee ya Qur'ani

Kwa upande wake, Hujjatul Islam Mohammadi amesema Mashindano ya 34 ya Kimataifa ya Qur'ani Tukufu ya Iran mwaka huu ni ya aina yake na ya kipekee duniani kwani ni mara ya kwanza kwa mashindano matano tafauti kufanyika wakati moja. Amesema mbali na yale ya kawaida ya wanaume kutakuwa pia na mashindano maalumu ya wanawake, watu wenye ulemavu wa macho, ya wanachuo wa vyuo vya dini na pia mashindano ya wanafunzi wa shule. Ameongeza kuwa, kauli mbiu ya mashindano ya kimataifa ya Qur'ani nchini Iran ni "Kitabu Kimoja Umma Moja" na kuongeza kuwa mada hii imetokana na mafundisho ya Qur'ani Tukufu.

Mashindano hayo ya Qur’ani yataendelea kwa muda wa siku sita ambapo kuna washiriki 276 kutoka nchi 83 duniani. 

3591344


captcha