IQNA

Qarii wa Misri: Kila mshiriki ni mshindi mashindano ya Qur'ani

18:45 - April 22, 2017
Habari ID: 3470946
TEHRAN (IQNA)-Qarii mtajika na mtaalamu wa Qur'ani kutoka Misri amesema kila mshiriki katika mashindano ya Qur'ani ni mshindi.

Ustadh Taha Abdulwahab, ambaye ni jaji katika Mashindano ya 34 ya Kimataifa ya Qur'ani Tukufu ya Iran, katika mahojiano maalumu na IQNA amesema: "Daima nawafahamisha washiriki wote, wawe wanashiriki katika kitengo cha kuhifadhi au qiraa kuwa hawapaswi kuwa na wasiwasi kuhusu matokeo kwani katika mashindano ya Qur'ani hatuna aliyeshindwa bali wote ni washindi."

Ustadh Abdulwahab ambaye anatathmini uwezo wa washiriki katika Sawt na Lahn ametoa wito kwa wanaoshindana wasiwe na wasiwasi na badala yake wawe makini katika ubora.

Amesema katika siku ya kwanza ya mashindano haya ya Iran baadhi ya washiriki walikuwa na wasiwasi na hivyo hawakuweza kuonyesha ubora wao kikamilifu.

Mtaalamu huyo wa Qur'ani kutoka Misri ameitaja nara ya mashindano ya mwaka huu ya "Kitabu Kimoja Umma Moja" kuwa ni ya kipekee katika mjumuiko huu wenye kuleta umoja wa Kiislamu. Aidha amesema kwa ujumla mashindano ya Qur'ani huwa na nafasi muhimu katika kuleta umoja miongoni mwa Waislamu.

Ustadh Abdulwahab ambaye ni qarii mashuhuri na mtajika nchini Misri pia ana Shahada ya Uzamifu (PhD) katika sayansi za Qur'ani kutoka Chuo cha Masomo ya Qur'ani mjini Beirut.

Mashindano ya 34 ya Kimataifa ya Qur'ani Tukufu ya Iran yalianza Jumatano na yataendelea kwa muda wa siku sita hapa Tehran hadi tarehe 25 Aprili (27 Rajab) katika Ukumbi wa Sala wa Imam Khomeini MA ambapo kuna washiriki 276 kutoka nchi 83 duniani.


captcha