IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema

Adui akishambulia Iran atapata jibu kali, hataweza kuainisha mwisho wa vita

9:58 - May 11, 2017
Habari ID: 3470975
TEHRAN (IQNA)-Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa: "Sawa na miaka ya nyuma, kwa kutegemea hima, jitihada, ubunifu na vipawa vyake, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itaendelea na mkondo wake wa 'nguvu ya kuzuia hujuma'.

Ayatullah Sayyed Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameyasema hayo leo Jumatano mjini Tehran wakati aliposhiriki katika hafla ya kuhitimu wanachuo wa Chuo Kikuu cha Kijeshi  cha Imam Hussein AS na kuongeza kuwa: "Lengo la sera ya 'nguvu ya kuzuia ya mfumo wa Kiislamu' ni kuwazuia wanaotumia mabavu kimataifa kuishambulia Iran." Ameongeza kuwa, "Maadui wafahamu kuwa, iwapo watafikia natija ya kuishambulia Iran, basi watakumbana na jibu kali sana kwani wanaweza kuwa waanzishaji lakini mwisho hautakuwa mikononi mwao."

Ayatullah Khamenei ameashiria nukta zinazolipa taifa na nchi ya Iran nguvu  na kusema: "Usalama na utulivu uliopo Iran katika eneo lenye migogoro ni moja ya fakhari kubwa za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na madola ya kiistikbari yanalenga kuvuruga usalama huo."

Kiongozi Muadhamu ameongeza kuwa, "elimu na ustawi wa kisayansi, "uchumi wenye nguvu na wenye kujitegemea," "nguvu za kijeshi" na "vikosi vya ulinzi" ni nukta ambazo zimepelekea Iran kuhesabiwa kama dola lenye nguvu. Amebaini kuwa,  daima adui amekuwa akichukizwa na nukta ambazo zimeipa nguvu Jamhuri ya Kiislamu.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesistiza kuwa, 'nguvu za kijeshi ni moja kati ya sababu kuu za uwezo mkubwa na kuongeza kuwa uwezo wa kimakombora wa Jamhuri ya Kiislamu utaongezwa na utalindwa kwa nguvu.

Ayatullah Khamenei pia amebainisha maudhui ya "serikali ya kimuqawama au ya kimapambano' na kusema: "Msimamo wa serikali ya kimuqawama ni kuwa na nguvu na uwezo wa kumzuia adui." Amesema Leo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kama serikali ya kimuqawama imeweza kuwa na usawishi kieneo na kimataifa kutokana na sera zake pamoja na uwezo wake wa kijeshi na kiuchumi.

Kiongozi Muadhamu pia amebainsiha malengo ya muda mfupi na muda mrefu  ya maadui wa mfumo wa Kiislamu na kusema malengo ya muda mrefu ya adui, muda wa kati na muda mfupi ni kubadilisha msingi wa mfumo wa Kiislamu, kutoa pigo kwa uchumi, maisha ya wananchi na usalama wa Iran.

Ayatullah Khamenei pia ameashiria uchaguzi utakaofanyika 19 Mei nchini Iran na kusema: "Iwapo wananchi watajitokeza katika uchaguzi na kuhudhuria huko kuwe kumeandamana na nidhamu, maadili sambamba na kuzingatia mipaka ya Kiislamu na kisheria, basi bila shaka uchaguzi huo utauleletea mfumo wa Kiislamu heshima na nguvu. Lakini iwapo uchaguzi utakumbwa na uvunjaji sheria na ukiukaji maadili basi adui atapata matumaini na hilo litakuwa kwa madhara yetu sote."

3598176

captcha