IQNA

Madrassah za Qur'ani zaenea nchini Eritrea

23:05 - May 18, 2017
Habari ID: 3470984
TEHRAN (IQNA)-Madrassah za jadi za kufunza Qur'ani nchini Eritrea zinaendelea kufunza Qur'ani kwa mbinu za kale huku zikizidi kuenea katika nchi hiyo ya kaskazini mashariki mwa Afrika.

Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA, Eritrea ni sehemu ya Habeshi (Abyssinia) ya kale na hivyo Uislamu unaaminika kufika katika nchi hiyo wakati wa uhai wa Mtume Muhammad SAW. Kwa msingi huo Uislamu una historia ndefu katika nchi hiyo ya Kiafrika. Tokea zama za kale Waislamu nchini humo walianzisha madrassa za kuhifadhi Qur'ani na kufundisha mafundisho ya kimsingi ya Uislamu.

Aidha madrassah hizo pia hufunza lugha ya Kiarabu, nahau, fiqhi, hisabati na baadhi ya sayansi za kidini. Wengi wanaofuzu katika madrassah hizo huelekea katika nchi jirani ya Sudan kwa ajili ya masomo ya juu ya kidini.

Waislamu wa Eritrea pamoja na kuwa si Waarabu lakini ni maarufu kwa usomaji bora wa Qur'ani hasa kwa mbinu ya Tartil.

Madrassah za jadi za kufunza Qur'ani nchini Eritrea ni maarufu kama 'Al Quran' na hutumia mbinu ya kale zaidi ya kufundisha katika nchi hiyo. Kwa hakika madrassah hizo ni sehemu ya turathi tajiri ya Kiislamu ambayo hushuhudiwa katika miji mbali mbali ya nchi hiyo. Madrassah hizo zina nafasi muhimu katika malezi sahihi ya watoto Waislamu nchini Eritrea na hutegemewa sana na jamii ya Waislamu nchini humo. Ni nadra kumpata kijana Mwislamu Eritrea ambaye hajawashi kusoma katika Madrassah hizo ambazo wanafunzi wake wote husoma wakiwa wamekaa katika mazulia au mikeka.

Jina la Eritrea lilitungwa mnamo mwaka 1890 na wakoloni wa Italia kutokana na neno la Kigiriki "erythraîa" linalomaanisha "bahari nyekundu”. Hii ni kwa sababu Bahari ya Shamu iliitwa "Sinus Erythraeus" na mabaharia Wagiriki au "Mare Erythraeum” kwa Kilatini na Waroma wa kale – maana yake ni "bahari nyekundu" – kwa Kiingereza "Red Sea”.

3600250

captcha