IQNA

Vyombo vya habari vya Kiarabu vyakiri

Kushiriki kwa wingi wananchi katika uchaguzi wa rais Iran

12:00 - May 20, 2017
Habari ID: 3470986
TEHRAN (IQNA)-Vyombo vya habari vya Kiarabu vimekiri kushiriki kwa wingi Wairani hasa wanawake katika uchaguzi wa rais wa awamu ya 12 wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Kushiriki kwa mamilioni wananchi wa Iran katika uchaguzi wa jana Ijumaa wa rais na mabaraza ya Kiislamu ya miji na vijiji kumeakisiwa kwa wingi na vyombo vya habari vya nchi za Kiarabu ambavyo vimevutiwa na hamasa iliyoibuliwa na Wairani katika uchaguzi huu.

Tovuti ya Al Youm al Sabii ya Misri imeakisi kushiriki wanawake katika uchaguzi wa jana Iran na kuandika: "Wanawake walishiriki kwa wingi katika uchaguzi wa rais nchini Iran.” Tovuti hiyo imechapisha taswira za wanawake wakiwa wanapiga kura na kuandika kuwa zaidi ya watu milioni 40 walishiriki katika uchaguzi huo wa rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Tovuti ya habari ya Al Arabi Al Jadid ya Misri pia imeandika kuwa muda wa kupiga kura uliongezwa mara kadhaa kutokana na idadi kubwa ya wapiga kura. Aidha tovuti hiyo imeandika kuwa, aghalabu ya wapiga kura mjini Tehran walimpigia kura rais Hassan Rouhani anayetetea nafasi yake katika duru ya pili huku wakaazi wa vijiji na miji midogo wakimpigia kura mshindani wake wa karibu Sayyed Ibrahim Raisi.

Vyombo vya habari vya Lebanon kama vile Al Manar, Al Mayadin na Al Ahd vyote vilikuwa na matangazo ya moja kwa moja kuhusu uchaguzi wa Iran ambapo vimeripoti kuwa kushiriki kwa wingi Wairani katika uchaguzi ni nembo ya demokrasia. Televisheni ya Al Mayadeen imetangaza kuwa zaidi ya asilimia 70 ya wapiga kura Iran walishiriki katika uchaguzi huo na kuutaja kuwa kati ya uchaguzi uliowashirikisha watu wengi zaidi katika historia ya Iran.

Mwandishi wa Al Jazeera naye aliakisi habari ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu akipiga kura mapema Ijumaa mjini Tehran. Aidha mwandishi wa Al Jazeera ametuma ripoti akiwa katika mji wa Qum na kuutaja mji huo kuwa mji mkuu wa kimaanawi Iran ambapo idadi ya wapiga kura ilikuwa ya juu sana.

Kwa ujumla kushiriki kwa wingi wananchi wa Iran katika uchaguzi wa rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni jambo ambalo limetajwa na vyombo vya habari vya Kiarabu kuwa nembo adhimu ya kidemokrasia.

Matokeo rasmi na kamili ya uchaguzi bado hayajatangazwa lakini hadi sasa kwa mujibu wa kura zilizohesabiwa Rais Rouhani amepata kura 22,796,468 huku nafasi ya pili ikishikiliwa na Ibrahim Raisi, akiwa amepata 15,452,194. Matokeo hayo ya awali ni kwa mujibu wa kura 40,076,729 zilizopigwa ambapo kura 38,914,470 zilikuwa sahihi. Matokeo kamili na rasmi yatatangazwa baadaye.

Tume uchaguzi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, imemtangaza Rais Hassan Rouhani kuwa mshindi wa duru ya 12 ya uchaguzi wa rais iliyofanyika Ijumaa kwa kupata kura milioni 23 ambazo ni sawa na asilimia 57. Huku Sayyid Ibrahim Raeisi akishika nafasi ya pili kwa kupata kura milioni 15 ambayo ni sawa na asilimia 38.5. Viongozi mbali mbali duniani wanaendelea kumtumia Rais Rouhani asalamu za pongezi kufuatia ushindi wake katika uchaguzi wa rais.


3601233

captcha