IQNA

Jeshi la Iran laangamiza mamia ya magaidi katika hujuma ya makombora Syria

12:56 - June 19, 2017
Habari ID: 3471025
TEHRAN (IQNA)-Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu Iran limetekeleza shambulizi la makombora na kulenga ngome za magaidi wa ISIS au Daesh nchini Syria ambapo mamia ya magaidi wameangamizwa.

Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA, duru zinadokeza kuwa, makombora hayo ya Iran yaliyovurumishwa jana usiku yalifanikiwa kulenga ngome ya ISIS nchini Syria.

Taarifa za awali zinasema kwa magaidi wamepata hasara kubwa sana ambapo hadi sasa 360 wamethibitika kuuawa huku vifaa vyao vingi vya kivita vikiharibiwa.

Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu IRGC limetangaza kuvurumisha makombora kadhaa ya balistiki hadi katika ngome ya magaidi wa ISIS katika eneo la Deir Ezzor nchini Syria kama njia ya kuwaadhibu magaidi waliohusika na hujuma za hivi karibuni mjini Tehran.

Taarifa ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu imesema: "Kufuatia jinai za magaidi hivi karibuni mjini Tehran ambapo watu 18 madhulumu waliuawa shahidi na wengine kujeruhiwa wakiwa katika saumu, IRGC ilitangaza kuwa, haitakaa pasina kujibu umwagaji damu takasifu."

Taarifa hiyo imeongeza kuwa: "Katika kuwaadhibu magaidi wakufurishaji nchini Syria, IRGC imetumia makombora ya masafa ya kati ya nchi kavu kwa nchi kavu na kulenga kamandi na eneo la mjumuiko wa magaidi na kituo cha kuunda magari ya deraya cha magaidi wa kitakfiri katika eneo la Deir Ezzor mashariki mwa Syria."

Kufuatia oparesheni hiyo iliyofana, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu limewaonya magaidi wakufurishaji na waungaji mkono wao katika eneo na nje ya eneo kuwa, iwapo watarudia tena hujuma na maovu yao dhidi ya taifa la Iran basi watakumbwa na ghadhabu na moto wa ulipizaji kisasi wa jeshi hilo.Jeshi la Iran laangamiza mamia ya magaidi katika hujuma ya makombora Syria

Taarifa zinasema IRGC ilivurumisha makombora hayo ya balisitiki jana usiku kutoka miji ya Sanandaj na Kermanshah magharibi mwa Iran hadi nchini Syria. Makombora hayo yaliyotumiwa yana uwezo wa kulenga shabaha umbali wa kilomita 800.

3611064

captcha