IQNA

Mapinduzi katika Ufalme wa Saudia, mfalme akiuka taratibu na kumteua mwanae kumrithi

10:45 - June 22, 2017
Habari ID: 3471031
TEHRAN (IQNA)- Mfalme Salman wa Saudia Jumatano alimtimua mrithi wa kiti chake na kumkabidhi nafasi hiyo mwanaye Muhammad bin Salman katika hatua iliyotajwa kuwa ni mapinduzi katika utawala.

Kwa muda mrefu sasa kumekuwepo na tetesi za migongano mikubwa katika safu za kiutawala katika ukoo unaotawala nchi hiyo wa Aal Saud. Tokea siku chache zilizopita duru za kisiasa zilimekuwa zikizungumzia harakati za Mfalme Salman bin Abdul Aziz wa nchi hiyo za kumuandalia mtoto wake huyo nafasi ya kuchukua madaraka katika siku zijazo na ndio maana akafanya mabadiliko makubwa katika mfumo wa utawala wa nchi hiyo katika miezi ya hivi karibuni, ambapo alikuwa amempunguzia madaraka Mohammed bin Nayef. Katika kuendeleza mabadiliko hayo, Mfalme Salman pia alikuwa amewateua washauri wake wapya wanne, wawili kati yao wakiwa wanatoka katika ukoo wa Aal Sheikh ambao ni wa Muhammd bin Abdul Wahhab, mwanzilishi wa pote potovu la Uwahabi. Ni muhimu kuashiria hapa kwamba mabadiliko hayo ya kiutawala nchini Saudi Arabia yamefanyika kufuatia mgogoro na kukatwa uhusiano wa nchi hiyo na Qatar ambao wajuzi wa mambo wanasema Mfalme Salman ameutumia kukabiliana na mahasimu wake wa kisiasa nchini humo.

Trump nyuma ya pazia mabadiliko Saudia

Ni wazi kuwa mabadiliko hayo ya kiutawala yana uhusiano wa moja kwa moja na safari ya hivi karibuni ya Rais Donald Trump wa Marekani katika nchi hiyo ya Kiarabu. Baadhi ya wataalamu wa mambo wanaamini kuwa moja ya malengo ya Mfalme Salman ya kualika na kumpokea kwa shangwe Rais Donald Trump na kisha kufunga naye mikataba mikubwa ya kijeshi na kiuchumi iliyoigharimu nchi hiyo mamia ya mabilioni ya dola, ilikuwa ni kumshawishi afumbie macho mabadiliko hayo. Wimbi kubwa la mabadiliko ya kisiasa nchini Saudia katika siku za hivi karibuni bila shaka linaonyesha kwamba Mfalme Salman anaharakisha hatua za kuhodhi kikamilifu madaraka ya nchi hiyo na kuitumbukiza zaidi katika fikra potovu za Uwahabi. Kuna uwezekano mkubwa wa mabadiliko hayo kuzidisha harakati za kupindukia mipaka, za uingiliaji na zisizo na busara za Saudi Arabia katika ngazi za kimataifa. Hii ni katika hali ambayo hatua ya mfalme huyo ya kumuuzulu Mohammed bin Nayef na kumuweka mahala pake mwanawe Muhammad bin Salman bila shaka itaongeza mivutano na vita vya kuwania madaraka nchini humo.

Mfalme Salman akiuka taratibu za ukoo

Ndio maana Mfalme Salman akachukua hatua za kuharakisha mabadiliko mengine makubwa katika nyanja za siasa na usalama wa nchi hiyo ili kukabiliana na uwezekano wa kutokea aina yoyote ya malalamiko kutoka kwa wale wanaoamini kwamba amevunja kanuni, sheria na mila za kukabidhiana madaraka na kuhodhi utawala nchini humo. Hatua za Mfalme Salman tokea achukue madaraka ya nchi hiyo zimekuwa zikienda kinyume kabisa na sheria na desturi zilizozoeleka katika nchi hiyo ya kifalme, jambo ambalo bila shaka litakuwa na matokeo mabaya kwa mfumo unatowala nchini humo. Mtoto wa Salman amekabidhiwa nafasi ya Mrithi wa Kiti cha Ufalme katika hali ambayo kwa mujibu wa sheria na wasia uliochwa na Mfalme Abdul Aziz, muasisi wa ukoo wa Aal Soud, madaraka yanapaswa kukabidhiwa kwa ndugu katika tabaka la watoto wake kabla ya kukifikia kizazi cha tatu cha watoto wao. Ukoo wa Aal Soud umekuwa ukiitawala Saudia tokea mwaka 1932 na daima kumekuwepo na vita vya kuwania madaraka katika ukoo huo.

Malalamiko na kusambaratika ukoo wa Aal Saud

Ni muhimu kukumbusha hapa kuwa mfumo wa utawala Saudia unadhibitiwa na mirengo miwili muhimu ya ukoo wa Shimri na ukoo wa Sudairi, mirengo ambayo huvutana vikali kwa ajili ya kuwania madaraka. Kati ya wafalme sita ambao wameitawala nchi hiyo tokea mauti yamfike Mfalme Abdul Aziz, watatu kati ya wafalme hao akiwemo mfalme wa hivi sasa Salman, wanatoka katika ukoo wa Sudairi. Kwa hivyo kama ufalme wa nchi hiyo utaendelea kubakia mikononi mwa ukoo wa Sudairi kupita Muhammad bin Salman ni wazi kuwa suala hilo halitakubalika na ukoo wa Shimri na hivyo kuwa chanzo cha vita vipya wa kuwania madaraka katika ukoo mkuu wa Aal Soud. Tayari malalamiko yaliyokuwa yakiendelea chini kwa chini kuhusiana na hatua ya Mfalme Salman kuhodhi madaraka ya Saudia yameanza kusikika hadharani na hakuna shaka kuwa huu utakuwa mwanzo wa kuanza kusmabaratika hatua kwa hatua ukoo unaochukiwa wa Aal Saud na hatimaye watu wa ardhi hiyo ya Hijaz iliyopacihkwa jina la Saudia waweze kupata haki ya kuainisha mustakbali wao kwa uhuru.

3612007


captcha