IQNA

Waislamu Kenya wajadili mtaala wa shule za Kiislamu na hatari ya misimamo mikali

19:45 - June 23, 2017
Habari ID: 3471032
TEHRAN (IQNA)-Waislamu nchini Kenya wanaendelea kujadili mtaala katika shule za Kiislamu maarufu kama Madrassah huku kukitolewa tahadhari ya kuingizwa misimamo mikali ya kidini katika mtaala huo.

Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA, Baraza Kuu la Waislamu nchini Kenya SUPKEM limetoa wito wa kuandaliwa mfumo mmoja wa masomo kwa ajili ya shule za Kiislamu katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki. Katika mkutano wake uliofanyika hivi karibuni katika msikiti wa Jamia jijini Nairobi, SUPKEM imesisitiza kwamba, kuna haja ya kuandaliwa mfumo mmoja wa masomo kwa ajili ya shule za Kiislamu nchini humo tofauti na sasa ambapo kila adrassha imekuwa na mfumo wake wa masomo.

SUPKEM imezitaka taasisi zote za masomo na utafiti za Kiislamu nchini Kenya ziandae mfumo mmoja jumuishi wa masomo katika viwango vyote katika shule za Kiislamu na kukabidhi kwa Wizara ya Elimu kama mpango wa masomo kwa ajili ya shule za Kiislamu.

Huku hayo yakijiri, Baraza Kuu la Masufi Afrika Mashariki limepinga baadhi ya sehemu za mtaala uliopendekezwa kutumika katika madrassah nchini humo.

Mwenyekiti wa baraza hilo Sheikh Abdukadir Adnan amesema Waislamu wenye misimamo mikali wameuteka mtaala wa Madrassah na iwapo utaidhinishwa, basi misimamo mikali itaongezeka nchini humo. Akizungumza Jumanne katika eneo la Mambrui karibu na mji wa Malindi katika pwani ya Kenya, Sheikh Adnan alisema Baraza la Masufi Afrika Mashariki linawakilisha asilimia 80 ya Waislamu Kenya huku makundi ya wenye misimamo mikali (Mawahhabi) wakiwa ni asilimia 20 tu.

Alisema baraza hilo litatumia uwezo wake kuhakikisha kuwa Uislamu halisi unawakilishwa katika mtaala wa masomo ya Madrassah. Kwa upande wake, mwanazuoni maarufu wa Kisufi Sheikh Abdulkadir Al-ahdi amesema wana mkakati wa kukabiliana na misimamo mikali kwa kuhubiri amani katika kaunti zote za Kenya. Amesema hawataruhusu vijana Waislamu waingizwe katika misimamo mikali ya kidini na uraibu wa dawa za kulevya. Wanazuoni wa Kiislamu katika Baraza la Masufi Afrika Mashariki wanasema misimamo mikali ya kidini inachochewa na Uwahhabi ambao chimbuko lake ni Saudi Arabia.

Mwaka 2012 serikali ya Kenya ilizitambua rasmi shule za Kiislamu au Madrassah zinazoendeshwa na kufundishwa kulingana tarataibu za wasimamizi.

3612095

captcha