IQNA

13:06 - July 02, 2017
News ID: 3471045
TEHRAN (IQNA)-Imebainika kuwa katika gereza moja lililo katika mji mkuu wa Tanzania, Dar es Salaam wamejaa mahafidh wa Qur ‘anI Tukufu wakitumikia kifungo, wengine
Mahafidh wa Qur’ani Tukufu wamejaa Gereza la Ukonga, Tanzania

Kwa mujibu wa gazeti la kila wiki la An Nuur, linalochapishwa nchini Tanzania, hayo yamebainika hivi karibuni katika kumi la mwisho la Mfungo wa Mwezi wa Ramadhani, baada ya wafungwa na mahabusu Waislamu katika Gereza la Ukonga kujitosa katika mashindano ya kuhifadhi Qur’an.

Mashindano hayo yaliandaliwa na Baraza Kuu la Waislamu wa Gereza la Ukonga kwa kushirikina ma waalimu wanaosomesha Qur’ani tukufu gerezani humo.

Taarifa zinasema mashindano hayo yalishirikisha Waislamu (wanafunzi) wapatao arobaini ambao ni wafungwa na mahabusu wa kutoka katika Mabweni (Cello) saba, zilizomo katika Gereza hilo.

Mashindano hayo yaliyozingatia vigezo vyote, yaliratibiwa na kusimamiwa na majaji sita ambao miongoni mwa hao, watatu walitoka katika ngome ya Bush na watatu toka ngome Tela.

Katika mashindano hayo, Majaji walitoa vigezo vya kuzingatia ili kumpata mshindi ambapo walizingatia kwanza Hukma za usomaji pamoja na kujiamini kwa msomaji, na pili sauti ya msomaji kama inasikika vizuri, akidhihirisha kila harufu.

Hali hiyo imewastajaabisha baadhi ya Waislamu wanaofika katika gereza hilo kwa ajili ya kuwaona ndugu na jamaa zao na kupata taarifa ya mashindani hayo ndani ya gereza.

Ustadhi Saidi Ally, alisema amestuka kusikia ndani ya gereza hilo kuna wafungwa waliohifadhi Qur’ani na kuisoma kwa ufasaha pamoja na kusema kuwa inafurahisha’ lakini pia akasema inatia huzuni ndani yake.

"Aaah, sitaki kusema mengi maana jambo hili ukilitafakari kwa kina unajiuliza maswali mengi ambayo majibu yake huwezi kuyapata kwa haraka, niseme tu inafurahisha na kuhuzunisha.” Amesema Ustadhi Ally.

Bi. Kudrat Mbwana, alisema amesikia taarifa kuwa kulifanyika mashindano ya kusoma na kuhifadhi Qur’ani gerezani, akahoji, "je, hawa waliingia wakiwa tayari wana Qur’an vifuani mwao au wamejifunzia wakiwa humo gerezani”.

Kwa upande wake Katibu wa Kamati ya Maafa ya Shura ya Maimamu, wanaoshughulikia Waislamu walipo Magerezani, Ustadhi Ally Mbaruku, alithibitisha kufanyika mashindano hayo.

Alisema ni kweli mashindano hayo yalifanyika japo hakueleza kwa undani washindani hao walishindanishwa katika Juzuu ngapi na aina gani ya zawadi walizopewa.

Alishindwa kufafanua zaidi juu ya suala hilo kwa kuzingatia masharti ya Gerezani.

Alisema, hali hiyo inatia moyo kuona kwamba waliopo magerezani wanaithamini Qur’ani kwani pamoja na kwamba alipatikana mshindi wa kwanza mpaka wa arobaini, kwa kuzingatia vigezo walivyo weka, lakini kwa ujumla wote ni mahafidhi.

"Kitendo tu cha kuingia katika mashindano tayari wewe ni mwenye kuhifadhi Qur’ani, sasa haijalishi umekuwa katika nafasi ya ngapi, unaweza ukawa umehifadi lakini sauti yako sio nzuri, hivyo haina maana kuwa huyo hajui,” amesema.

Ustadhi Mbaruku, alisema Waislamu hao walimpa ujumbe wakisema kwamba wanawaomba ndugu zao Waislamu walio uraiani kuwaunga mkono kwa kuwapelekea juzuu na misahafu ili waweze kuisomesha Qur’ani ambayo inaweza kuwaongoa ili wakitoka humo wawe ni watu wa aina nyingine kabisa.

Katika mashindano hayo, walioshika nafasi ya kwanza mpaka ya tano ni Salimu Ismail wa kwanza aliyepata asilimia 96, pili ni Hamadi Hamad, aliyepata asilimia 88, watatu alikuwa Ussy Mtumwa, aliyepata asilimia 84, wanne ni Mbaraka Hassan, alama 80 na nafasi ya tano likwenda kwa Maksud Seif, aliyepata alama alama 80.

Chanzo: Gazeti la An Nuur
Name:
Email:
* Comment: