Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran pia amezungumzia mzingiro wa Israel dhidi ya watu wa eneo la Ukanda wa Gaza na kusema, mzingiro huo ni jinamizi kubwa kwa wakazi wa eneo hilo ambalo linapaswa kushughulikiwa. Zarif amesema kuwa, utawala wa Kizayuni wa Israel umepuuza matakwa yote ya jamii ya kimataifa kwa ajili ya kusitisha na kubadili siasa zake za kibaguzi dhidi ya watu wa Palestina.
Tarehe 14 mwezi uliomalizika wa Julai Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel aliliamuru jeshi la utawala huo haramu kufunga milango yote ya kuingia na kutoka katika Msikiti wa al Aqsa huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu kwa siku kadhaa, suala lililozusha machafuko makubwa na kupelekea kuuawa raia kadhaa wa Palestina.
Wapalestina 15 wameuawa shahidi na wengine wapatao 1,400 wamejeruhiwa katika matukio ya karibuni ya msikiti wa Al-Aqsa na katika duru mpya ya mapigano kati ya waandamanaji wa Kipalestina na askari wa Kizayuni yaliyoanza tarehe 14 a Julai huko Ufukwe wa Magharibi wa Mto Jordan, Quds tukufu na Ukanda wa Gaza.
Hatua ya kichochezi ya utawala wa Kizayuni ya kuifunga milango ya msikiti wa Al-Aqsa iliamsha hasira za Waislamu kote duniani.