IQNA

Televisheni ya kwanza ya Kiislamu Kenya yazinduliwa

23:04 - August 16, 2017
Habari ID: 3471125
TEHRAN (IQNA)-Msikiti wa Jamia mjini Nairobi umezindua televisheni ya kwanza ya Kiislamu nchini Kenya.

Televisheni hiyo iliyopewa jina la Horizon TV ilizinduliwa rasmi Ijumaa iliyopita katika sherehe iliyohudhuriwa na mwenyekiti wa Kamati ya Msikiti wa Jamia Sheikh Osman Warfa.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Warfa alisema televisheni hiyo inalenga kuondoa taswira potovu kuhusu Uislamu na Waislamu na wakati huo huo kuhimiza mazungumzo na maelewano baina ya Wakenya wote.

Nchini Kenya tayari kuna televisheni kadhaa za Kikristo kama vile Family TV na GBS na hivyo kuanzishwa televisheni ya Kiislamu ni hatua muhimu kwa jamii ya Waislamu nchini humo kuweza kutangaza dini yao tukufu.

Horizon TV, ambayo imekuwa ikirusha matangazo kwa miezi kadhaa, inalenga kuwa nguzo ya taifa la Kenya na itakuwa na vipindi vya kuelimisha vya kidini na vya kawaida.

Mwenyekiti wa kamati ya kuratibu uendeshaji wa teelvisheni hiyo, Profesa Abdullatif Essafee anasema: "Tutalenga kuwasilisha taswira chanya kuhusu Waislamu na Wakenya sambamba na kuwaelimisha na kuwatumbiza watazamaji wetu kwa njia ambayo haikiuki maadili na misingi ya Kiislamu.”

3463668
captcha