IQNA

Hatimaye Saudia yaruhusu mahujaji wa Qatar

0:34 - August 18, 2017
Habari ID: 3471128
TEHRAN (IQNA)- Hatimaye baada ya mashinikizo, Saudi Arabia imeafiki kufungua mpaka wake wa pamoja wa ardhini na Qatar kuruhusu mahujaji kutoka nchi hiyo kuelekea kwenye ardhi tukufu za Makka na Madina kwa ajili ya kutekeleza ibada ya Hija ya mwaka huu.

Shirika rasmi la habari la Saudia limeeleza kuwa mpaka wa Salwa uliofunguliwa leo utakuwa wazi kwa ajili ya kupita raia wa Qatar wanaotaka kwenda kuhiji pasi na kuhitajia vibali vya elektroniki.

Uamuzi huo umechukuliwa kufuatia safari ya Sheikh Ahmad bin Abdullah bin Jasim Al Thani, mwanamfalme wa Qatar huko nchini Saudia na mazungumzo aliyofanya na mrithi wa ufalme wa nchi hiyo Muhammad bin Salman.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar Sheikh Mohammed bin Abdulrahman Al Thani amekaribisha hatua hiyo lakini amesisitiza kuwa Hija haipasi kutumiwa kisiasa na kwamba uamuzi huo ungepasa kujumuisha pia uondoaji kikamilifu wa vikwazo vyote vya kisiasa na kiuchumi ilivyowekewa nchi yake na Saudi Arabia na nchi nyengine tatu washirika wa Riyadh.

"Bila kujali namna raia wa Qatar walivyozuiliwa kutekeleza Hija, hatua ambayo ilichukuliwa kisiasa, na namna walivyoruhusiwa tena kuhiji ambako pia kumefanyika kisiasa... serikali ya Qatar inakaribisha uamuzi huo na itautolea jibu chanya", ameongezea kusema waziri huyo.

Mpaka wa Salwa, ambao ni mpaka pekee wa ardhini kwa Qatar ulikuwa umefungwa tangu Saudi Arabia, Misri, Bahrain na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) zilipovunja uhusiano wao wa kidiplomasia na serikali ya Doha Juni 5 mwaka huu zikiituhumu kuwa inaunga mkono ugaidi, tuhuma ambazo Qatar imezikanusha.

Kamati ya Taifa ya Haki za Binadamu ya Qatar (NHCR) nayo pia imekaribisha uamuzi huo wa Saudia wa kufungua mpaka wake lakini imesema hauko wadhiha bali una utata hususan kuhusiana na mahujaji wanaoishi nchini Qatar. Taarifa iliyotolewa na kamati hiyo hii leo imetaka utendeaji na utoaji huduma uwe sawa kwa mahujaji wote bila ya ubaguzi wala upendeleo. Saudi Arabia pia mwaka jana iliwazuia raia wa Iran, Syria na Yemen kushiriki katika ibada ya Hija.

3463678/

captcha