IQNA

Waislamu Uingereza wataka gazeti la The Sun lichukuliwe hatua

9:56 - August 23, 2017
Habari ID: 3471137
TEHRAN (IQNA)-Baraza la Waislamu Uingereza linataka gazeti la The Sun nchini humo lichukuliwe hatua kwa kuandika makala yenye kuchochea hisia dhidi ya Waislamu.

Kauli hiyo imekuja baada ya makala iliyoandikwa na Trevor Kavanagh kudai kuwa Uingereza ina ‘Tatizo la Waislamu’. Makala hiyo iliashiria kuwa Waislamu wanapaswa kuangamizwa kwa kutumia mbinu za Ujerumani ya Kinazi..

Baraza Huru la Viwango vya Vyombo Habari Uingereza tayari limepokea malalamiko zaidi ya 150 kutokana na kauli ya gazeti hilo lenye wasomaji wengi Uingereza na sasa inasubiriwa kuona ni hatua gani zitakazochukuliwa. Pamoja na hayo weledi wa mambo wanasema ni vigumu hatua kali zichukuliwe dhidi ya gazeti hilo kwa kuzingatia kuwa chuki dhidi ya Uislamu ni jambo ambalo limekita mizizi katika taasisi nyingi za serikali na zisizo za serikali nchini Uingereza.

Gazeti la The Sun, ambalo lina wasomjai takribani milioni 5 kwa wiki, lina historia ya kuandika makala dhidi ya Waislamu., Mwaka 2015 gazeti hilo lililazimika kuomba radhi baadhi ya kuandika kuwa katika kila Waislamu watano Uingereza moja anaunga mkono ugaidi.

Kwa mujibu wa sensa ya hivi karibuni ya watu Uingereza, kuna Waislamu milioni 2.8 nchini humo kati ya watu milioni 64 nchini humo.

Pamoja na mchango wao mkubwa na wa kihistoria nchini Uingereza, Waislamu wanakabiliwa na changamoto nyingi hasa kubaguliwa na kutengwa na watu wenye misimamo mikali ya utaifa na chuki dhidi ya Uislamu.

3471001

captcha