IQNA

Msikiti Uholanzi wahujumiwa na wenye chuki dhidi ya Uislamu

11:52 - September 03, 2017
Habari ID: 3471155
TEHRAN (IQNA)-Msikiti ambao ungali unajengwakusini mashariki mwa Uholanzi umeshambuliwa na watu wenye misimamo mikali ya chuki dhidi ya Uislamu.

Hujuma hiyo imetekelezwa na wafuasi wa kundi lenye misimamo mikali ya mrengo wa kulia la ‘Identitair Verzet’ ambao wamepachika mabango yaliyo na maandishi yenye dhidi ya Uislamu katika paa la Msikiti wa Tevhid (Tauhid) ambao ungali unajengwa katika mji wa Venlo. Mkuu wa Msikiti wa Tevhid amezungumza na waandishi habari Jumamosi na kulaani kitendo hicho huku akisema pamoja na kuwa kuna wafuasi wengi wa makundi ya misimamo ya kufurutu ada, hakutaraji wangetekeleza hujuma kama hiyo.

"Tumezungumza na meya wa mji na maafisa wengine na wanatuunga mkono," amesema na kuongeza kuwa: "Tutachukua hatua za kuzuia vitendo kama hivyo siku za usoni."

Kundi la ‘Identitair Verzet’ limetangaza kuhusika na hujuma dhidi ya msikiti huo ambao ulikuwa umepachikwa mabango kama vile, "Tokeni hap, Uholanzi ni Yetu", "Hatutaki Msikiti na Waislamu Katika Mtaa Wetu."

Maandishi hayo yaliandikwa kwa Kiholanzi na Kituruki kutokana na kuwa idadi kubwa ya Waislamu katika eneo hilo wana asili ya Uturuki.

Waislamu nchini Ulaya wamekuwa wakishuhudia ongezeko la hujuma za watu wenye chuki dhidi ya Uislamu katika miaka ya hivi karibuni huku Uholanzi ikiwa moja kati ya nchi zinazolengwa zaidi.

3637662

captcha