IQNA

Rais wa Iran asisitiza ulazima wa kusaidiwa Waislamu wa Myanmar

9:57 - September 08, 2017
Habari ID: 3471163
TEHRAN (IQNA)- Rais Hassan Rouhani wa Iran amesisitiza kuhusu ulazima wa kusaidiwa Waislamu wa jamii ya Rohingya wanaokandamizwa na kuuawa kwa umati nchini Myanmar.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema utumiaji silaha ya mauaji ya kimbari hauwezi kukubalika katika dunia ya leo na kusisitiza kwamba hakuna tofauti yoyote kati ya Waislamu wa Myanmar na Waislamu wengine duniani. Akizungumza katika kikao cha Baraza la Mawaziri Jumatano, Rais Hassan Rouhani aliongeza kuwa, "Nchini Myanmar Waislamu wa jamii ya Rohingya wanakumbwa na matatizo na zaidi ya watu laki moja ima wameuawa au wamekuwa wakimbizi. Maiti za baadhi yao zimeteketezwa, nyumba zao zimechomwa moto. Sisi kama Waislamu, na kama nchi ya kimapinduzi inayowaunga mkono waliodhulumiwa duniani hata kama si Waislamu, tunapaswa kuwasaidia Waislamu wa Myanmar."

Wakati huo huo Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameitaka jamii ya kimataifa kuchukua hatua za kivitendo za kukomesha uangamizaji wa kizazi wanayofanyiwa Waislamu wa kabila la Rohingya na mabudha wa Myanmar.

Mohammad Javad Zarif alisisitiza hayo Alhamisi katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Tweeter na kuongeza kuwa, hakuna kitu chochote kinachoweza kuhalalisha kimya cha jamii ya kimataifa mbele ya mauaji ya kimbari wanayofanyiwa Waislamu wa Rohingya.

Misaada ya Iran tayari kwa ajili ya Waislamu Myanmar

Huku hayo yakijiri Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kuwa misaada ya Jamhuri ya Kiislamu kwa Waislamu wa Rohingya huko Myanmar iko tayari kutumwa na kwamba Tehran inafanya juhudi za kuhakikisha misaada hiyo inawafikia Waislamu hao wanaonyanyaswa na kudhulumiwa kinyama.

Ibrahim Rahimpour amesema hayo Alhamisi usiku na kuongeza kuwa, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Mohammad Javad Zarif amemwandikia barua Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na kutaka mgogoro wa Waislamu wa Rohingya ujadiliwe wiki ijayo katika kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Ijumaa ya tarehe 25 Agosti lilianza wimbi jipya la mashambulizi ya kikatili ya jeshi la Myanmar na Mabudha dhidi ya Waislamu wasio na ulinzi wa Rohingya katika mkoa wa Rakhine wa magharibi mwa Myanmar ambapo duru zinasema hadi sasa Waislamu zaidi ya 3,000 wameangamizwa kwa umati. Halikadhalika tangu wakati huo hadi hivi sasa zaidi ya Waislamu laki moja na 70 elfu wamekimbia makazi yao.

Mwaka 2012 jeshi la Myanmar lilianzisha mashambulizi mapya ya kikatili dhidi ya Waislamu wa kabila la Rohingya na hadi hivi sasa serikali ya mabudha ya nchi hiyo inawanyima Waislamu hao haki zao za kimsingi kabisa kama vile uraia.

3639310

captcha