IQNA

Katika Hotuba Umoja wa Mataifa
15:37 - September 21, 2017
News ID: 3471185
TEHRAN (IQNA)-Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amehutubu katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na kuitahadharisha Marekani kuhusu hatua yoyote ya kukiuka mapatano ya nyuklia ya Iran.

Akizungumza Jumatano mjini New York katika mkutano mkuu wa 72 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA), Rais Rouhani aliongeza kuwa, miamala ya kijahili, michafu, chuki na iliyokosa uelewa sambamba na utoaji tuhuma zisizokuwa na msingi wowote ya Rais Donald Trump wa Marekani dhidi ya taifa la Iran wakati akihutubu katika umoja huo si tu kwamba, haiendani taratibu za Umoja wa Mataifa, bali inakinzana pia na matakwa na matarajio ya leo ya watu wa mataifa yote ya dunia katika kikao hicho.

Aidha ameashiria uvunjaji mikataba wa Marekani katika njia ya utekelezaji wa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na kusema kuwa, uvunjaji huo wa mikataba ya kimataifa unaivunjia heshima na itibari Washington yenyewe. Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa kuheshimiwa haki za binaadamu na haki za kiraia kando na kushikamana na Uislamu na uadilifu, ni kati ya matakwa muhimu ambayo yalisisitizwa sana na raia wa Iran kipindi cha kabla ya mapinduzi ya Kiislamu ya Iran.

Rais Rouhani pia amelaani ukandamizaji wa utawala haramu wa Kizayuni wa Israel kwa kusema, ni suala lisilokubalika kwa raia wa Palestina kuendelea kunyimwa haki zao za kimsingi na utawala wa shari na ghasibu wa Kizayuni.

Ameongeza kwa kusema, ni suala lisilowezekana kwa baadhi ya watu kudhani kuwa inawezekana kufikiwa ustawi na maisha bora kwa nchi mbalimbali katika hali ambayo bado Waislamu wa Yemen, Syria, Iraq, Bahrain, Afghanistan, Myanmar na maeneo mengine ya dunia wanaendelea kukabiliwa na hali mbaya sana ya umasikini, ukandamizaji, vita na machafuko katika nchi zao.

Amefafanua zaidi kwa kusema kuwa kuheshimiwa huko kwa haki za binaadamu na haki za kiraia na kadhalika kushikamana na Uislamu na uadilifu ni mambo ambayo yamekuwa yakisisitizwa na Wairan katika kipindi chote cha historia kwa zaidi ya miaka 150 iliyopita hususan katika kipindi cha kujiri mapinduzi ya Kiislamu ya mwaka 1979.

Aidha amezungumzia ushiriki mkubwa wa wananchi katika medani ya kisiasa na kusema kuwa, katika kipindi cha miezi minne iliyopita na katika duru ya 12 ya uchaguzi wa rais, zaidi ya Wairan milioni 41 walifika katika masanduku ya kupigia kura na kwa mara nyingine wakathibitisha uaminifu wao kwa siasa za msimamo wa wastani, kuheshimu haki za binaadamu na haki za uraia katika siasa za ndani nchini Iran. Amesema kuwa upigaji kura huo haukuwa ni wa kumchagua rais pekee, bali uwekezaji mkubwa wa kisiasa wa wananchi ambao ndio waungaji mkono wakubwa kwa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Rais wa Iran alibainisha kwa kusema kuwa: "Msimamo wetu ni kupigania amani na kuunga mkono haki za mataifa mengine. Hatukubali dhulma, lakini pia tunamtetea mtu anayedhulumiwa. Hatutoi vitisho lakini pia hatukubali vitisho vya mtu yeyote, lugha yetu ni lugha ya heshima na kwa ajili hiyo hatukubaliani na lugha yoyote ya vitisho."

3644302


Name:
Email:
* Comment: