IQNA

19:11 - September 22, 2017
News ID: 3471186
TEHRAN (IQNA)-Waislamu barani Ulaya wanahisi kuongezeka ubaguzi ambapo wawili kati ya watano (asilimia 40) wakisema wamekumbana na ubaguzi wakati wa kutafuta kazi, nyumba au huduma za umma kama vile elimu an matibabu.

Kwa mujibu wa ripoti mpya, karibu asilimia 30 ya waliohojiwa wanasema wamewahi kutusiwa na asilimia mbili wamehujumiwa kimwili katika kipindi cha miezi 12 kabla ya uchunguzi huo ambao umefanywa na Idara ya Haki za Kimsingi ya Umoja wa Ulaya (EU Fundamental Rights Agency).

Uchunguzi huo ulifanyika kuanzia mwishoni mwa mwaka 2015 hadi mapema 2016 na ulijumuisha Waislamu 10,500 katika nchi 15 zikiwemo Ufaransa,Ujerumani, Uholanzi, Uhispania, Sweden na Uingereza.

Wengi ambao wamebaguliwa katika kipindi cha miaka mitano kabla ya uchunguzi huo wanahisi walibaguliwa kwa sababu ya jina, rangi ya ngozi au dhahiri yao. Karibu asilimia 17 wanasema walihisi kubaguliwa kwa sababu ya itikadi zao za kidini hii ikiwa ni ongezeko la asilimia saba kutoka wakati wa uchunguzi kama huo uliofanyika mwaka 2008.

Karibu asilimia 40 ya wanawake Waislamu ambao huvaa Hijabu, ima mtandio au niqabu hadharani wanahisi vazi lao ndio sababu ya kubaguliwa wakati wa kutafuta kazi. Aidha asilimia 30 ya wanawake ambao huvaa Hijabu wanasema walibughudhiwa au kutusiwa.

Asilimia 12 ya Waislamu waliobaguliwa na asilimia 9 waliochkozwa waliripoti matukio hayo. Aidha asilimia 47 ya wanaume waliosimamishwa na polisi barabarani wanasema wanahisi walisimamishwa kwa ajili ya mavazi yalioyoonekana kuwa ni ya Kiislamu.

Mkuu wa Idara ya Haki za Kimsingi ya Umoja wa Ulaya Michael O’Flaherty anasema kila kitendo cha ubaguzi au hujuma ya chuki hupunguza uwezekano wa Waislamu kupata ajira na hivyo hupelekea watengwe zaidi na jambo hilo ni hatari kwa nchi husika.

Ripoti hiyo inasema Waislamu ni karibu asilimia 4 ya watu wote barani humo na kwamba asilimia 78 wanasema wanaufungamano wa kizalendo na nchi wanamoishi huku asilimia 92 wakisema hawana tatizo kuishi na majirani wasio Waislamu. Baadhi ya duru zinasema idadi ya Waislamu barani Ulaya ni asilimia 7.66 au watu milioni 56 kati ya watu takribani milioni 740 barani humo.

Name:
Email:
* Comment: