IQNA

11:29 - September 26, 2017
News ID: 3471194
TEHRAN (IQNA)-Msikiti umeteketezwa moto katika mji wa Orebro kusini mwa Sweden katika tukio ambalo linaaminika kutekelezwa na watu wenye chuki dhidi ya Uislamu.
Msikiti wateketezwa moto SwedenTaarifa zinasema msikiti huo uliteketezwa moto usiku wa kuamkia Jumanne na kwamba wazimamoto walipowasili ulikuwa umeteketea kikamilifu.

Mkuu wa zimamoto katika mji wa Orebro Bw. Ulf Jacobsen anasema hakuna aliyejeruhiwa katika tukio hilo na kwamba ushahidi unaonyesha kuwa moto huo uliwashwa kwa makusudi.

Msikiti wa Orebro ulijengwa mwaka 2007 katika mtaa wa Vivalla ambao ni makazi ya wahajiri Waislamu kutoka nchi mbali mbali.

Tukio hilo limekuja baada ya msikiti mwingine kuteketezwa moto katika eneo la Jakobsberg ambalo ni kitongoji cha mji mkuu wa Sweden, Stockholm.Msikiti wateketezwa moto Sweden

Uchunguzi uliofanywa na Baraza la Ushirikiano wa Kiislamu Sweden mwaka 2015 ulibaini kuwa misikiti saba kati ya 10 nchini humo imehujumiwa na watu wenye chuki dhidi ya Uislamu.

Sweden ni nchi ambayo kwa muda mrefu imekuwa mwenyeji wa wahajiri na hivi sasa asilimia 15 ya wakazi wake walizaliwa nje ya nchi hiyo.

Hivi karibuni mwanasiasa wa cha chama cha Democrats nchini Sweden alwakasirisha wengi kwa kuivunjia heshima Qur’ani Tukufu.

Mattias Karlsson kiongozi wa bungeni wa chama cha Sweden Democrats (SD), ambacho kinapinga wahajiri kutoka nchi za Waislamu, hivi karibuni alitoa matamshi ya yenye chuki na kudai kuwa eti Qur’ani Tukufu ni sawa na kitabu cha ‘Mein Kampf’ (Mapambano Yangu) kilichoandikwa na Adolf Hitler mwaka 1925 akibainisha mitazamo yake ya kisiasa.

Karlsson ni muungaji mkono wa Rais Donald Trump wa Marekani ambaye aliwahi kusema kuwa Sweden inakabiliwa na mgogoro kutokana na kuwepo Wahajiri wengi Waislamu. Matamshi kama hiyo yamekuwa yakichochea hujuma dhidi ya Waislamu Sweden na maeneo mengine katika nchi za Magharibi.

Idadi ya Waislamu Sweden inakadiriwa kuwa zaidi ya laki sita kati ya watu milioni 9.9 katika nchi hiyo ya eneo la Scandinavia barani Ulaya.

3646580/

Name:
Email:
* Comment: