IQNA

11:47 - September 28, 2017
News ID: 3471196
TEHRAN (IQNA)-Mtafiti mmoja nchini Misri amesema mkataba aliofunga Bwana Mtume Muhammad SAW na Wakristo ni hati ya kwanza kuhusiana na kuheshimu dini tofauti duniani.

Abdul Rahim Rayhan, mkurugenzi mkuu wa kituo cha tafiti na mitaala ya mambo ya kale katika eneo la kaskazini mwa Misri amesema, mkataba aliofungiana Mtume SAW na Wakristo ambao taswira ya nakala yake ya asili imehifadhiwa kwenye maktaba ya jengo la watawa la Saint Catherine lililoko kwenye mlima wa Sinai nchini Misri ni hati ya kwanza ya kimataifa kuhusiana na kuheshimu dini za wengine.

Mtafiti huyo wa Kimisri amefafanua kwamba kwenye mkataba huo imeelezewa misingi na kanuni za kuyahami na kuyalinda matukufu ya Wakristo na kutoa msaada wa kuyakarabati na kuyafanyia matengenezo na vile vile kutoyatusi na kuyavunjia heshima matukufu yao.

Abdul Rahim Rayhan aidha ametoa wito wa vifungu vya mkataba huo kusomeshwa na kubainishwa katika mikutano ya kimataifa ya suluhu na amani na katika makongamano ya wafuasi wa dini mbalimbali.

Inasemekana kuwa matini ya mkataba aliofungiana Bwana Mtume Muhammad SAW na Wakristo ilisomwa na mtukufu huyo na kuandikwa na Imam Ali AS  ndani ya msikiti mtukufu wa Mtume SAW katika mji wa Madina.

3645684

Name:
Email:
* Comment: