IQNA

Waislamu katika maombolezo ya siku ya Ashura duniani

9:11 - October 01, 2017
Habari ID: 3471200
TEHRAN (IQNA) Siku ya leo inasadifiana na mwezi 10 Muharram 1439 Hijria, siku ya kukumbuka wakati damu ilipoushinda upanga kwa ushujaa wa Imam Hussein AS na wafuasi wake wachache katika jangwa la Karbla la Iraq ya leo.
Waislamu katika maombolezo ya siku ya Ashura dunianiSiku kama ya leo miaka 1378 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, moja kati ya vita mashuhuri katika historia ya Kiislamu na ya mwanadamu, vilitokea baina ya majeshi ya haki na batili katika ardhi ya Karbala huko Iraq.

Siku hii inajulikana kwa jina la Ashura. Katika siku hiyo mjukuu wa Mtume Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib AS, alisimama kishujaa na wafuasi wake waaminifu 72, kukabiliana na jeshi kubwa la batili ili kuilinda dini ya Allah.

Hamasa ya Karbala ilikuwa dhihirisho la mambo mawili makuu. Kwanza ni ujasiri, ushujaa, moyo wa kujitolea, uaminifu pamoja na kuyapokea kwa moyo mkunjufu mauti ya kuuawa shahidi, sifa walizojipamba nazo wapiganaji wachache wa jeshi la haki wakiongozwa na Imam Hussein AS dhidi ya Yazid bin Muawiya.

Mtukufu huyo AS alitangaza wazi kwamba lengo lake la kuanzisha mapambano hayo lilikuwa ni kuamrisha mema na kukataza mabaya pamoja na kuhuisha mafundisho na thamani za dini ya Mtume Mtukufu SAW.

Pili ni upeo wa ukatili, udhalimu na unyama ulioonyeshwa na jeshi batili la Yazid bin Muawiya. Baada ya kupambana kishujaa na jeshi hilo kubwa la Yazid, hatimaye mjukuu huyo wa Mtume Muhammad SAW aliuawa shahidi katika siku kama ya leo.

Waislamu, hasa wafuasi wa Madhebu ya Shia na wale wawapendao Ahul Bayt wa Mtume SAW, leo wanashiriki katika hafla mbali mbali za maombolezo ya Imam Hussein AS. Aidha hata wasio kuwa Waislamu katika maeneo mbali mbali pia wanajumuika na Waislamu katika maombolezo ya Imam Hussein AS kwani aliuawa shahidi akitetea haki na kupinga udhalimu.

Shirika la Habari la IQNA linatoa mkono wa pole kwa Waislamu na wapenda haki wote na hasa wapenzi wa Bwana Mtume Muhammad SAW na watu wa nyumba yake toharifu kwa kukumbuka tukio hilo la chungu na la kusikitisha ambalo katu halitasahaulika.

Hapa tunakumbusha hadithi ya Bwana wetu Mtume Muhammad SAW aliposema: "Kwa hakika kifo (shahada) cha (Imam) Hussein kitaamsha mori (harara) katika nyoyo za waumini ambao hautapoa milele."

3647836


Waislamu katika maombolezo ya siku ya Ashura duniani

Waislamu katika maombolezo ya siku ya Ashura duniani

Waislamu katika maombolezo ya siku ya Ashura duniani


captcha