IQNA

Mwanafunzi Marekani avuliwa Hijabu na mwalimu wake wa kiume

15:42 - November 18, 2017
Habari ID: 3471269
TEHRAN (IQNA)-Mwalimu mmoja wa kiume katika jimbo la Virginia Marekani ameadhibiwa kwa likizo ya lazima baada ya kupatikana na hatia ya kuivua Hijabu ya mwanafunzi wake Mwislamu.

Mwanafunzi huyo amesimulia kisa hicho katika ukurasa wake wa Twitter na kusema Jumatano iliyopita Hijabu yake ilivutwa kutoka katika kichwa chake na mwalimu ambaye alikuwa akimheshimu.

Anasema alikuwa anazungumza na rafiki yake wakati ghalfa mwalimu huyo aliyekuwa nyuma yake alipovua Hijabu. Mwanafunzi huyo anasema alistaajabu wakati mwalimu huyo alipomwambia, "nywele yako inapendeza."

Idara ya Shule za Umma katika eneo la Fairfax County imetoa taarifa na kusema tukio hilo halifai na halikubaliki na kwamba uchunguzi umeanzishwa huku mwalimu aliyehusika akilazimishwa kuenda likizo.

Baraza la Mahusiano ya Uislamu na Marekani CAIR, ambalo hutetea maslahi ya Waislamu nchini humo, limetoa taarifa na kusema, "Tunapongeza hatua ya kuadhibiwa kwa likizo ya lazima mwalimu aliyehusika. Pia tunapongeza hatua ya mwalimu kumuomba radhi mwanafunzi na familia yake, lakini hatua zaidi za kinidhamu zinapaswa kuchukuliwa kwa mujibu wa matokeo ya uchunguzi wa tukio hilo linalotia wasiwasi," amesema Nihad Awad mkurungezi mtendaji wa CAIR. Ameongeza kuwa hakuna mwalimu anayepaswa kubughudhiwa au kuhujumiwa kwa ajili ya Imani yake. Walimu wanapaswa kuwalinda wanafunzi ni si kuwa chanzo cha kuwakera na kuwasumbua.

Katika miezi ya hivi karibuni kumeripotiwa vitendo vya walimu na wanafunzi kuwavua Hijabu wanafunzi Waislamu katika shule mbali mbali kote Marekani, nchi ambayo imeshuhudia ongezeko maradufu la chuki dhidi ya Waislamu tokea Donald Trump achukue hatamu za urais mwezi Januari mwaka huu.

3464453

captcha