IQNA

Ujumbe wa OIC kutembelea kambi za wakimbizi Waislamu Warohingya nchini Bangladesh

11:37 - January 02, 2018
Habari ID: 3471340
TEHRAN (IQNA)-Ujumbe wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) umepanga kutembelea kambi za wakimbizi Waislamu wa jamii ya Rohingya katika mji wa Cox’s Bazar nchini Bangladesh kuanzia Januari 3-6.

Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA, ujumbe huo unajumuisha wanachama wa Tumu Huru ya Haki za Binadamu ya OIC pamoja na maafisa wa idara ya Masuala ya Kibinadamu na Jamii za Waliowachache katika OIC.
Safari hiyo imepangwa kwa ushirikiano na serikali ya Bangladesh kwa lengo la kutathmini hali ya haki za binadamu na maisha ya wakimbizi Waislamu wa jamii ya ROhingya ambao wametoroka ardhi yao ya jadi nchini Myanmar kufuatia hujuma zinazotekelezwa dhidi yao na jeshi la nchi hiyo pamoja na Mabudhha wenye misimamo mikali ya kidini.
Wakuu wa Myanmar wamekataa ombo la OIC la kuruhusu maafisa wa haki za binadamu kuenda katika jimbo la Rakhine kuchunguza hali ya Waislamu wanaokandamizwa katika jimbo hilo. Ripoti kamili kuhusu hali ya Waislamu Warohingya itkabidhiwa baraza la mawaziri wa mambo ya nje wa nchi za OIC ambao wanatarajiwa kukutana mjini Dhaka, Bangladesh mwezi Mei mwaka huu.
Jinai kubwa wanazofanyiwa Waislamu hao na wanajeshi na Mabudha wa nchi hiyo  wenye misimamo ya kufurutu katika mkoa wa Rakhine magharibi mwa Myanmar  tangu tarehe 25 mwezi Agosti mwaka huu; hadi sasa zimepelekea kuuliwa Waislamu zaidi ya elfu sita na kujeruhiwa maelfu ya wengine huku zaidi ya laki sita wakilazimika kuwa wakimbizi katika nchi jirani ya Bangladesh.
Hivi karibuni Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa alisema kuwa uhalifu unaofanywa na Mabudha kwa himaya ya serikali nchini Myanmar dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya ni mauaji ya kimbari.
Zeid Ra'ad Al Hussein alisisitiza katika kikao cha Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa lililokutana kujadili hali ya Waislamu wa Rohingya katika jimbo la Rakhine huko Myanmar kwamba, kuna udharura wa kufika katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo na kufanya uchunguzi kuhusu ukatili unaofanywa na serikali ya Myanmar dhidi ya Waislamu.
Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa alisema kuwa kutotambua haki za watu wa jamii ya Rohingya kama kaumu yenye haki na heshima ni kuwadunisha na kuwadhalilisha Waislamu wa Myanmar.
Ra'ad Al Hussein amesema kuwa, Waislamu wa Rohingya wanalengwa na kuuawa kwa sababu ya utambulisho wao na kwamba wananyimwa hata haki ya kuwa na majina ya Kiislamu.

3464834

captcha