IQNA

Magaidi wa Boko Haram wameua Waislamu 5,000 katika jimbo moja nchini Nigeria

12:16 - January 03, 2018
Habari ID: 3471341
TEHRAN (IQNA)-Magaidi wakufurishaji wa Boko Haram wameuawa Waislamu 5,247 katika jimbo la Adamawa nchini Nigeria kati ya mwaka 2013 na 2017, ripoti ya shirika moja la Kiislamu imefichua.

Kwa mujibu wa taarifa, Tawi la Jimbo la Adamawa la Baraza la Waislamu limesema maeneo yaliyoathiriwa na hujuma hizo za Boko Haram ni pamoja na Madagali, Michika, Maiha, Mubi North, Mubi South, Hong na Gombi.
Ripoti iliyotiwa saini na mwenyekiti wa baraza hilo Abubakar Magaji imesema Waislamu wengine 5,161 walijeruhiwa katika hujuma hizo za magaidi wakufurishaji wa Boko Haram.
Halikadhalika ripoti hiyo imesema kuwa mali 12,732 za Waislamu ikiwemo misikiti, shule nyumba, mifugo na mazao ya kilimo yenye thamani ya dola milioni 2.2 iliharibiwa katika hujuma za magaidi wa Boko Haram.
Ripoti hiyo ilipendekeza kukarabatiwa upya misikiti na shule za Kiislamu zilizoharibiwa na magaidi wa Boko Haram huku wito ukitolewa kwa serikali kuimarisha usalama na kuwapa misaada ya kifedha waathirika wa jinai za kundi hilo la kigaidi.
Adamawa ni kati ya majimbo matatu yaliyoathiriwa vibaya na ugaidi wa Boko Haram kaskazini mwa Nigeria, mengine yakiwa ni Borno na Yobe.
Tokea Boko Haram ianzishe uasi wake Nigeria mwaka 2009, watu elfu 20 wamepoteza maisha. Aidha zaidi ya watu milioni mbili wamefanywa wakimbizi kufuatia ugaidi wa Boko Haram.
Neno Boko Haram kwa lugha ya Kihausa lina maana ya 'elimu kutoka nchi za Magharibi ni haramu'. Kundi hilo la Boko Haram ambalo lina ufahamu usio sahihi na potovu kuhusu dini ya Kiislamu, limekuwa likitekeleza hujuma katika maeneo mbalimbali ya Nigeria hasa kaskazini mwa nchi hiyo.
Mwaka 2015 magaidi hao wakufurishaji wa Boko Haram walipanua wigo wa hujuma zao hadi katika nchi jirani za Niger, Cameroon na Chad.

3678051

captcha