IQNA

Waislamu Korea Kusini warahisishiwa njia ya kupata chakula Halali

12:00 - January 18, 2018
Habari ID: 3471359
TEHRAN (IQNA)-Waislamu nchini Korea Kusini sasa wamerahisishiwa njia za kupata chakula halali kupitia aplikesheni ya simu za mkononi ijulikanyao kama Crave Halal ambayo pia ina tovuti ya intaneti.

Aplikesheni hiyo ya Crave Halal inalenga kuwawezesha Waislamu wa Korea Kusini na wageni Waislamu, hasa watakaoshiriki katika Michezo ya Olimpiki ya Msimu wa Baridi 2018 wapate chakula halali pasina matatizo.

Shirika la Crave Halal limefanya uchunguzi katika migahawa yote iliyorodheshewa ili kuhakikisha kuwa ina chakula halali kabla ya kuiorodhesha. Kwa kutumia aplikesheni au tovuti ya Crave Halal, watumizi wanaweza kupata migahawa halali karibu nao, kupata maelezo kuhusu wakati wa kufunguliwa na maelekezo ya kufika uliko mgahawa na kisha kutuma maoni yao baada ya huduma.

Idadi ya Waislamu Korea Kusini ni ndogo lakini mwaka 2016 karibu watalii milioni moja Waislamu walitembelea nchi hiyo.

Serikali ya nchi hiyo inalenga kuongeza idadi hiyo kwa asilimi 20 mwaka huu wa 2018 ambapo aghalabu ya Waislamu ambao hutembelea nchi hiyo ni kutoka Indonesia, Malaysia na Mashariki ya Kati.

Michezo ya Olimpiki ya Msimu wa Baridi 2018 inatazamiwa kufanyika kuanzua Februari 9-25 katika mji wa Pyeongchang Korea Kusini na inatabiriwa kuwa maelfu ya watalii Waislamu watakuwa miongoni mwa watazamaji.

3464960

captcha