IQNA

Msikiti wateketezwa moto tena Washington, Marekani

20:24 - March 22, 2018
Habari ID: 3471439
TEHRAN (IQNA)- Moto mkubwa umeteketeza na kuharibu tena Kituo cha Kiislamu cha Eastside katika eneo la Bellevue, jimbo la Washington nchini Marekani, hii ikiwa ni mara ya pili eneo hilo la Waislamu kuteketezwa moto katika kipindi cha mwaka moja.

Msemaji wa kituo cha Kiislamu cha Eastside Omar Lone amesema jengo hilo, linalojumuisha pia msikiti, limekuwa halitumiwi tokea lilipoteketezwa moto mara ya kwanza huku kukifanyika jitihada za kukusanya michango ya ukarabati. Lone amesema anaamini tukio la kutetekea moto jengo hilo ni la makusudi. Amesema kwa kuzingatia kuwa hakuna mtu aliyekuwa ndani na jengo limezungukwa na ua, pia kauna umeme wala gesi, hivyo kuna uwezekano mkubwa kuwa moto huo uliwashwa lengo la kutetekteza kikamilifu jengo hilo.

Mwezi Januari mwaka 2017, mtu aliyetambuliwa kama Wayne Wilson, 37, ambaye alidai hana makao, alipatikana na hatia ya kutekteza kituo hico cha Kiislamu mwezi Septemba mwaka 2016. Wilson alihukimiwa kifungo cha miezi 14 gerezani.

Polisi wanasema wangali wanachunguza tukio hilo la Jumatano.  Tukio hilo linajiri wakati vitendo vya chuki dhidi ya Waislamu vimeongezeka mno huko Marekani tangu Donald Trump aliposhika hatamu za uongozi zaidi ya mwaka moja uliopita.

Mwezi Disemba mwaka jana, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu Wa Umoja wa Mataifa, Zeid Ra'ad Al Hussein amekosoa hatua ya hivi karibuni ya Rais wa Marekani, Donald Trump aliyesambaza taswira zilizo na chuki dhidi ya Uislamu kupitia akaunti yake ya Twitter.

 Mwaka 2015, na kabla ya kujitosa kwenye kampeni za kuwania urais wa Marekani, alidai kuwa "Uislamu unaichukia Marekani." Wakati wa kampeni za uchaguzi Trump aliahidi kuwa endapo atashinda na kuingia Ikulu ya White House atawazuia Waislamu wasiingie nchini Marekani.

Kuna ushahidi kadhaa unaoonyesha kuwa Trump anajaribu kwa makusudi kuyafufua na kuyapa nguvu makundi ya kibaguzi na yenye misimamo ya kufurutu mpaka ndani na nje ya Marekani.

3465434

captcha