IQNA

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu

Watawala wa Marekani, Uingereza na Ufaransa waliohujumu Syria ni watenda jinai

23:59 - April 14, 2018
Habari ID: 3471465
TEHRAN (IQNA) Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameyataja mashambulizi yaliofanywa alfajiri ya leo na nchi za Marekani, Uingereza na Ufaransa dhidi ya Syria kuwa ni jinai na uhalifu na kusema kuwa: Marais wa Marekani na Ufaransa na Waziri Mkuu wa Uingereza ni wahalifu waliotenda jinai.

Ayatullah Ali Khamenei ameyasema hayo leo mjini Tehran katika hadhara ya maafisa wa serikali, mabalozi wa nchi za nje na wananchi wa matabaka mbalimbali waliohudhuria majlisi ya kusherehekea siku ya kupewa Utume Nabii Muhammad (saw). Amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itaendelea kuwa bega kwa bega na makundi ya wanamapambano, na hapana shaka kwamba Marekani itafeli na kushindwa katika malengo yake kwenye eneo la Mashariki ya Kati na kukumbwa na hatima ile ile ya Afghanistan an Iraq.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema mienendo ya Marekani na baadhi ya nchi za Magharibi inatokana na malengo yao ya kikoloni na udikteta wao wa kimataifa na kusisitiza kuwa: Madikteta katika eneo lolote lile la dunia hawawezi kufanikiwa na kupata ushindi; vivyo hivyo Marekani kamwe haitafikia malengo yake na itashindwa katika Mashariki ya Kati.

Amesema kuwa, lengo la Wamarekani si Syria, Iraq na Afghanistan pekee bali wanataka kutoa pigo kwa Umma wa Kiislamu na Uislamu; kwa msingi huo tawala za Waislamu hazipaswi kuhudumia malengo ya Marekani na baadhi ya nchi vamizi za Kimagharibi.

Ayatullah Khamenei amesema kuwa, sababu ya kuwepo Iran huko Syria na eneo la Asia magharibi ni kuwasaidia wanamapambano wanaokabiliana na dhulma na sasa kambi hiyo ya mapambano imefanikiwa kuyashinda makundi ya kigaidi yaliyoanzishwa na Marekani, Wamagharibi na vibaraka wao kama Saudi Arabia kutokana na msaada huo wa Iran na ushujaa wa jeshi la Syria.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, mahala popote watu wanaodhulumiwa watakapoomba msaada, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itakuwa tayari kwenda kuwasaidia na kwamba, hiyo ndiyo falsafa ya sisitizo la Jamhuri ya Kiislamu la kuwasaidia Wapalestina. Ameongeza kuwa: Taifa la Palestina sasa limekuwa taifa imara kutokana na kusimama kwake kidete na hapana shaka kuwa, Wapalestina watawashinda Wazayuni maghasibu na kurejesha ardhi ya Palestina kwa taifa hilo.

/3700204

captcha