IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu
20:57 - April 26, 2018
News ID: 3471483
TEHRAN (IQNA)- kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeendelea kusimama imara mbele ya dhulma za madola ya kibeberu na kiistikbari kwa kipindi cha miaka 40 sasa na imeendelea kupata maendeleo, uwezo na nguvu zaidi licha ya vinyongo vya maadui wanaotaka kuangamiza mfumo huo wa Kiislamu.

Ayatullah Ali Khamenei ameyasema hayo mapema leo Alhamisi mjini Tehran katika hadhara ya washiriki wa Mashindano ya Kimataifa ya 35 ya Kusoma na Kuhifadhi Qur'ani Tukufu ya Iran na kuongeza kuwa: “Njia pekee ya maendeleo na ufanisi wa Umma wa Kiislamu ni kutekeleza mafundisho ya Qur'ani”. Amesema kuwa, nchi za Kiislamu zimepatwa na maradhi ya "udhalili na kuwa duni" kutokana na kutoshikamana na Qur'ani tukufu na kwamba kauli ya Rais wa Marekani aliyesema bila ya haya kuwa "kama si Marekani basi baadhi ya nchi za Kiarabu hazitaweza kuendelea kuwepo kwa zaidi ya wiki moja", ni matokeo ya maradhi hayo.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, “Qur'ani Tukufu inatwambia, waumini wanapaswa kuwa na umoja na mfungamano wa kidugu na wasiwe na mfungamano wowote na kambi ya ukafiri; hata hivyo inasikitisha kuona kwamba, hii leo baadhi ya nchi za Waislamu zina mfungamano na mshikamano na utawala wa Kizayuni wa Israel, na matokeo ya hatua hiyo ya kutotekeleza maagizo ya Qur'ani ni vita na mauaji ya sasa katika eneo la Asia Magharibi.

Amewaambia washiriki wa mashindano ya Kimataifa ya Qur'ani mjini Tehran kwamba: "Hebu tazameni hali ya watu wa Yemen wanaoendelea kuzongwa na masibu makubwa na sasa harusi zao zimekuwa vikao vya misiba. Tazameni pia hali ya watu wa Afghanistan, Pakistan na Syria; haya yote ni matokeo ya kusahauliwa udugu na mfungamano baina ya waumini na kutotekelezwa mafundisho ya Qur'ani."

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa: Iwapo qiraa na usomaji wa Qur'ani tukufu utakuwa utangulizi wa kutekeleza mafundisho yake, hapana shaka kuwa mustakbali wa Umma wa Kiislamu utakuwa bora zaidi kuliko ilivyo hivi sasa na Marekani haitaweza tena kuzitisha nchi na Umma wa Kiislamu na kuwatwisha matakwa na masharti yake.

Kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Hujjatul Islam Mohammadi, Mkuu wa Shirika la Wakfu la Iran, ambalo liliandaa mashindano ya kimataifa ya Qur’ani, aliwasilisha ripoti kuhusu mashindano hayo na kusema: “Mashindano ya 35 ya Kimataifa ya Qur’ani Tukufu yalikuwa na jumla ya washiriki 380 kutoka nchi 84 duniani na miongoni mwa walikuwemo waliohifadhi Qur’ani, wasomaji wa Qur’ani, majaji wa mashindano, watafiti na wanazuoni wa Qur’ani Tukufu. Aidha kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu washiriki kadhaa wa mashindano hayo walisoma aya za Qur'ani Tukufu.

3709388

Name:
Email:
* Comment: