IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Umoja na Ustawi wa Kisayansi ni Mahitajio ya Umma wa Kiislamu Leo

22:05 - May 12, 2018
1
Habari ID: 3471509
TEHRAN (IQNA)- Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, harakati ya elimu katika Ulimwengu wa Kiislamu inapaswa kuwa na kasi kubwa na kwa mara nyingine tena Umma wa Kiislamu ufikie kilele cha nguvu za kielimu na kiustaarabu ili maadui wa Uislamu wakiwemo Wamarekani washindwe kutoa amri kwa marais wa nchi za Kiislamu kwa kuwaambia fanyeni hili na msifanye lile.

Ayatullah Ali Khamenei amesema hayo asubuhi ya leo mjini Tehran alipokutana na washiriki wa Kongamano la Kimataifa  la "Nafasi ya Ushia katika Kuleta na Kueneza Elimu za Kiislamu" na kusema kuwa, hitajio muhimu kabisa hii leo kwa Ulimwengu wa Kiislamu ni "Umoja na Mshikamano na vile vile kuweko "Harakati Kubwa Kwa Ajili ya Ustawi wa Kisayansi Katika Sayansi Zote".

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa, hii leo kumejitokeza "Mwamko" katika Ulimwengu wa Kiislamu na licha ya njama za Wamagharibi za kukana hilo, mwamko huu umeandaa uwanja zaidi wa watu kuelekea katika Uislamu na hivyo kuwa ni habari njema kwa ajili ya mustakabali.

Ayatullah Khamenei amesema kuwa, sababu kuu ya Ulimwengu wa Kiislamu kuwa chini ya ubeberu ni kubakia nyuma kielimu na kuongeza kuwa, baada ya Ulimwengu wa Magharibi kubakia nyuma kisayansi kwa karne kadhaa, umeweza kuyatumia maendeleo ya kisayansi ya Ulimwengu wa Kiislamu na kujiongezea utajiri, nguvu za kisayansi, kijeshi, kisiasa na kipropaganda na hatimaye kwa kutumia ukoloni Wamagharibi wameweza kuzifikisha nchi za Kiislamu katika hali ya kusikitisha ya hivi sasa.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria utumiaji mabavu wa madola ya Magharibi dhidi ya nchi za Kiislamu na akthari ya watawala wa nchi hizo kufuata utumiaji mabavu huo wa kimataifa na kusisitiza kwamba, hali hii inapaswa kubadilishwa kupitia maendeleo ya elimu na hivyo Ulimwengu wa Kiislamu kuweza kwa mara nyingine tena kufikia kilele cha ustaarabu wa mwanadamu.

Ayatullah Khamenei ameitaja Iran kuwa mfano wa kuigwa katika ustawi wa kisayansi na kuongeza kuwa, kasi ya ustawi wa Iran kisayansi ni mara 13 zaidi ya wastani wa kimataifa na hilo limethibitishwa katika ripoti za taasisi za kimataifa za sayansi.

Kiongozi Muadhamu amesisitiza kuwa, Iran itaendelea katika mkondo wake huu wa ustawi na kuongeza kuwa, kinyume cha madola ya Magharibi, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iko tayari kuzinufaisha nchi za Kiislamu na mafanikio yake ya kisayansi.

/3713521

Imechapishwa: 1
Inatathminiwa: 0
Haiwezi kuchapishwa: 0
Ntagungira Rashidi
0
0
Napenda sana kufuatiria habari kuhusu Taifa la Jamhuri ya Kiislam ya Iran, lakini habari nyingi zinapitishwa katika lugha ya Kingereza naomba muongeze mara dufu habari kuhusu Mashariki ya Kati katika lugha ya Kiswahili.

Ama kuhu maudhui haya yanayohusia a na sayansi ni kweri kwamba nchi za Kiislam zimebaki nyuma na hilo likawa chanzo cha kuburuzwa na kuendeshwa kimabavu kiyasi kwamba baadhi ya nchi za Kiislam zimeisha zoea kuendeshwa bila hata kutingisha bega zao

Ni vizuri sana iwapo mataifa ya Kiislam yatafuata na kusikia mwito huu wa Kiongozi mwadham Ayatullah Said Khamenei ambae ni Kiongozi mwenye kufaa na ni mkakamavu katika kuisimamia haki na kuifurusha batili, hivyo iwapo mataifa ya Kiislam na waislamu kwa ujumla wakifwata rai hii ya Kiongozi .mwenye busara na uelewa, hatunabudi waislam kujifungua minyiroro ya maadui wa Uislam na waislam, hivyo Mwenyezi Mungu Mtukufu ajarie akili zetu na uelewa wetu kuelewa vyema ushauri na rai ya Kiongozi mwema na mpenzi wa haki Inshaallah.
captcha