IQNA

Mahakama Bahrain yawahukumu kifungo cha maisha jela raia sita

20:17 - June 01, 2018
Habari ID: 3471539
TEHRAN (IQNA) - Mahakama ya utawala wa kidikteta wa Aal Khalifa imetoa hukumu ya kifungo cha maisha jela kwa raia sita wa Bahrain kwa kisingizio cha kushiriki kwenye machafuko yaliyotokea nchini humo.

Mahakama za kimaonyesho za utawala wa Aal Khalifa kila mara hutoa hukumu za adhabu ya kifo, vifungo vya muda mrefu jela au kuwavua uraia wanamapinduzi wa Bahrain kwa kuwafungulia kesi na mashtaka bandia.

Mashirika mbalimbali ya kimataifa hadi sasa yameshauonya mara kadhaa utawala huo wa kiimla kutokana na hatua zake za kushadidisha ukandamizaji dhidi ya wanaharakati wa kisiasa na kijamii.

Mnamo Jumatano ya tarehe 23 Mei, kituo cha haki za binadamu na demokrasia cha Bahrain kilitangaza kuwa katika kipindi cha miaka sita iliyopita utawala wa Aal Khalifa umewavua uraia wananchi 728 wa nchi hiyo.

Tangu Februari 14 mwaka 2011 hadi sasa, Bahrain imekuwa uwanja wa maandamano ya amani ya wananchi wanaopinga utawala wa kiukoo wa Aal Khalifa.

Wananchi hao wanataka kuwepo uhuru, utekelezwe uadilifu, ukomeshwe ubaguzi na kuundwa serikali itakayochaguliwa na wananchi wenyewe.

Hata hivyo kwa msaada wa wanajeshi wa Saudi Arabia na askari usalama wa Imarati waliotumwa nchini Bahrain kupitia mpango wa ulinzi wa Ngao ya Kisiwa, utawala wa Aal Khalifa unatumia mkono wa chuma kukabiliana na matakwa ya wananchi hao.

Kwa mujibu wa duru za haki za binadamu, Bahrain ina idadi kubwa zaidi ya wafungwa wa kisiasa kulinganisha na idadi ya watu katika nchi hiyo ndogo zaidi katika Ghuba ya Uajemi.

3465987

captcha