IQNA

Katibu Mkuu wa UN atembelea kambi ya wakimbizi Waislamu Warohingya Bangladesh

17:41 - July 03, 2018
Habari ID: 3471581
TEHRAN (IQNA)-Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametembelea kambi ya wakimbizi Waislamu wa jamii ya Rohingya huko Cox’s Bazar nchini Bangladesh na kusema alichoshuhudia kinamkumbusha wajukuu zake.

Amesema watoto hao Warohingya hawastahili kuishi maisha hayo, hivyo jamii ya kimataifa iongeze msaada.

Amesema simulizi za madhila waliyopitia watoto ikiwemo mateso, kubakwa na kukiukwa kwa haki zao ni tosha kusema kuwa warohingya ni kabila linalobaguliwa zaidi duniani ikizingatiwa kunyimwa utaifa na nchi yao Myanmar.

Katibu Mkuu amesema na baada ya machungu huko kwao sasa hata ukimbizini, “Pia ni jambo baya kwetu sisi kuona zaidi ya watu laki tisa wanaishi kwenye mazingira haya mabaya. Ninapoona watoto wa kiume na wa Kike nakumbuka wajukuu zangu wenyewe, na nafikiria kile ambacho kingalikuwa kushuhudia wajukuu zangu katika mazingira haya. Hii haikubaliki.”

Hivyo Guterres akasema kwa kuwa Bangladesh imejitolea kufungua mipaka yake kwa warohingya ni  lazima jamii ya kimataifa sasa ifungue mikoba yake akisema ombi la takribani dola bilioni moja kusaidia wakimbizi hao limechangia kwa asilimia 26 tu.

Kwa hivyo ombi lake kwa jamii ya kimataifa ni kuongeza zaidi msaada wa fedha kwa wale wote wanaofanya kazi nchini Bangladesh kusaidia na kuwalinda wakimbizi wa Rohingya.

Katibu Mkuu aliwasili Bangladesh siku ya jumamosi jioni ambapo jana jumapili alikuwa na mazungumzo na viongozi wa serikali akiwemo Waziri Mkuu Sheikh Hasina na pia kushiriki mkutano wa kujadili utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu, SDGS nchini humo.

Waislamu wa jamii ya Rohingya wamelazimika kukimbia kutoka ardhi zao za jadi nchini Myanmar na kutafuta hifadhi katika nji jirani ya Bangladesh kufuatia jinai kubwa wanazofanyiwa na wanajeshi na Mabudha wa nchi hiyo  wenye misimamo ya kufurutu katika mkoa wa Rakhine magharibi mwa nchi hiyo.

Wimbi jipya la jinai dhidi ya Waislamu Rarohingya  zilishika kasi tangu tarehe 25 mwezi Agosti mwaka jana. Hadii sasa  jinaI hizo zimepelekea kuuliwa Waislamu zaidi ya elfu sita na kujeruhiwa maelfu ya wengine huku wengine karibu laki nano wakilazimika kuwa wakimbizi katika nchi jirani ya Bangladesh.

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa uhalifu unaofanywa na Mabudha kwa himaya ya serikali nchini Myanmar dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya ni mauaji ya kimbari.

Zeid Ra'ad Al Hussein anasisitiza kwamba, kuna udharura wa kufika katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo na kufanya uchunguzi kuhusu ukatili unaofanywa na serikali ya Myanmar dhidi ya Waislamu.

3466200

captcha