IQNA

Kuhifadhi Qur’ani Huboresha Maisha ya Wenye Ulemavu wa Macho

22:14 - July 04, 2018
Habari ID: 3471582
TEHRAN (IQNA)-Hafidh wa Qur’ani mwenye ulemavu wa macho amesema kuhifadhi Qur’ani Tukufu huwasaidia wenye ulemavu wa macho kuishi maisha mazuri.

Katika mahojiano na IQNA, Abdullah Hamad Salim Hamad Abdu Shurayda amesema kuhifadhi Qur’ani huboresha maisha binafsi na ya kijamii ya mwenye ulemavu wa macho.

Abu Shurayda, ambaye hivi karibuni alishiriki katika Mashindano ya Kimataifa ya Wenye Uelmavu wa Macho nchini Iran, amesema wenye ulemavu wa macho huheshimiwa katika jamii wanapo hifadhi Qur’ani.

Ameongeza kuwa, kuhifadhi Qur’ani kumemsaidia yeye kujiboresha kimasomo shuleni na baadaye katika chuo kikuu na hivyo kumpa matumaini zaidi maishani.

Hafidh huyo wa Qur’ani kutoka Qatar pia ameyapongeza mashindano ya walemavu wa Qur’ani yaliyofanyika Iran na kusema ni miongoni mwa bora zaidi duniani. Amesema amewahi kuhudhuria mashindano ya Qur’ani Kuwait na Lebanon lakini yale ya Iran yalikuwa na usimamizi bora zaidi.

Abu Shurayda anasema ilimchukua miaka minne kuhifadhi Qur’ani Tukufu na kwamba kila siku yeye husoma juzuu tatu ili kuimarisha uwezo wake wa kuendelea kuhifadhi kitabu hicho kitakatifu.

Mashindano ya 35 ya Kimataifa ya Qur'ani Tukufu ya Iran (ya kawaida maalumu kwa ajili ya wanaume) na pia mashindano mengine ya Qur'ani ya wanawake, ya wenye ulemavu wa macho, ya wanafunzi wa shule na ya wanachuo wa vyuo vya kidini yalifanyika kati ya Aprili 19-15 katika miji ya Tehran, Qum na Mashhad nchini Iran.

3707433

captcha