IQNA

Saudia yamkamata mhubiri wa zamani wa Masjid An-Nabawi

12:48 - July 21, 2018
Habari ID: 3471602
TEHRAN (IQNA)- Utawala wa Saudi Arabia umemkamata mhubiri maarufu na mtetezi wa haki za binadanu Sheikh Ali bin Saeed al-Hajjaj al Ghamdi ambaye aliwahi kuwa mhubiri katika Al-Masjid An-Nabawi mjini Madina.

Taarifa katika mitandao ya kijamii zinasema Sheikh al-Ghamdi ametiwa mbaroni pamoja wanafunzi wake kadhaa ikiwa ni katika muendelezo wa kamatakmata ya wanazuoni wa kidini na watetezi wa haki za binadamu nchini Saudia katika miezi ya hivi karibuni.

Imedokezwa kuwa Sheikh al-Ghamdi, ndugu yake pamoja, wakili wake na wanafunzi wake watano wamekamatwa baada ya maafisa wa usalama kuhujumu nyumba yake.

Aidha duru zinaarifu kuwa Sheikh al-Ghamdi ambaye ana matatizo ya pumzi ametiwa kizuizini pasina maafisa wa usalama kumruhusu abebe kapsuli yake ya ozigeni. Ukamataji huu umejiri wiki moja baada ya  mwanazuoni mwingine mpinzani Sheikh Safar  al-Hawali  kukamatwa baada ya kuandika utangulizi katika kitabu cha 'Waislamu na Utamaduni wa Magharibi'. Kitabu hicho kina nasaha za wahubiri na maulamaa wa kidni kwa watawala wa ukoo wa Aal Saudi.

Wakati huo huo taarifa zinasema hali ya afya ya wanazuoni wanaoshikiliwa ni mbaya mno hasa Sheikh al-Hawali na Sheikh Salman al-Ouda wanaougua maradhi mbali mbali. Aidha idadi kubwa ya wafungwa hao wanateswa na haki zao zinakiukwa huku wakilazimishw akukiri kufanya makossa ambayo hawajafanya.

Vita vya madaraka katika ukoo wa Aal Sad nchini Saudi Arabia vinachukua mkondo mpya na mpana zaidi kila siku ambapo wanawafalme, wanazuoni na maafisa wengi wa ngazi za juu nchini humo wamekuwa wakitiwa mbaroni kwa amri ya Muhamm bin Salman, Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa nchi hiyo.

Tokea baba yake Salman bin Abdul Aziz, achukue kiti cha ufalme wa Saudia mnamo Junuari 2015, Muhammad bin Salman ambaye hakuwa akijulikana vizuri nchini humo ametokea kuwa mtu aliye na madaraka makubwa na anayechukua maamuzi yote muhimu ya kiserikali nchini. Uchu wa madaraka wa Bin Salman umekuwa ukiandamana na uvunjaji wa desturi na mila za nchi hiyo, mfano wa wazi ukiwa ni hatua yake ya kutwaa nafasi ya mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudia, kutoka kwa mrithi mstahiki wa nafasi hiyo na ambaye alikuwa angali hai yaani, Muhammad bin Naif.

Muhammad bin Salman anafanya kila analoweza ili kuwafuta washindani na wapinzani wake wote wanaoweza kumzuia kuchukua ufalme wa Saudia.

3731744

captcha