IQNA

Imran Khan ashinda uchaguzi Pakistan, asisitiza ushirikiano na Iran

20:04 - July 27, 2018
Habari ID: 3471609
TEHRAN (IQNA) Imran Khan, Mkuu wa chama cha Tehreek-e-Insaf (PTI) cha nchini Pakistan na kilichoshinda uchaguzi wa Bunge la nchi hiyo amesisitiza kuwa chama chache kinataka kustawisha uhusiano mwema na majirani zake ikiwemo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Akizungumza katika kikao cha kwanza na waandishi wa habari Alhamisi baada ya kutangazwa matokeo yasiyo rasmi ya uchaguzi wa Bunge uliofanyika Jumatano, Imran Khan amegusia siasa za nje za serikali ijayo ya Pakistan na kueleza kuwa: Nchi hiyo inahitajia amani na utulivu na kwamba serikali ijayo itaimarisha uhusiano wake na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.  

Mkuu huyo wa chama cha Tehreek-e-Insaf ameongeza kuwa Afghanistan ndiyo nchi iliyoathiriwa zaidi katika mapambano dhidi ya ugaidi kuliko nchi nyingine. Imran Khan amesema kuwa usalama wa Pakistan unategemea usalama wa nchi ya Afghanistan na kwamba pale nchi hiyo itakapokuwa na utulivu, Pakistan pia itakuwa katika hali ya usalama.

Wakati huo huo mchezaji huyo wa zamani wa kimataifa wa mchezo wa kriketi ameitaja Kashmir kuwa ni kadhia yenye umuhimu mkubwa katika uhusiano wa Pakistan na India na kueleza kuwa wakazi wa eneo hilo linalodhibitiwa na India wamekuwa walengwa wa ukiukaji wa haki za binadamu kwa zaidi ya miaka 30 sasa.

Sisitizo la Imran  Khan la kustawisha uhusiano wa Islamabad na Tehran ni ishara tosha kuhusu azma yake thabiti ya kuimarisha ushirikiano na Tehran kutokana na mchango na nafasi amilifu ya Iran katika kusaidia juhudi za kudumishwa amani katika eneo hili la Asia na vilevile nafasi ya Iran kama mshirika wa kweli wa kibiashara na kiuchumi wa Islamabad. Iran ambayo ni miongoni mwa nchi zinazozalisha nishati kwa wingi duniani, inaweza kuwa na nafasi yenye taathira chanya katika kukidhi mahitaji ya nishati ya Pakistan.

Japokuwa serikali zilizopita za Pakistan zilipiga hatua kiasi katika kustawisha ushirikiano na Tehran, lakini kurefuka kwa utekelezaji wa ujenzi wa bomba la gesi kutoka Iran hadi Pakistan katika miaka ya hivi karibuni ni ishara kwamba, Islamabad imeathiriwa na mashinikizo ya Marekani yanayoitaka ipunguze ushirikiano wake na Iran.

3733591

captcha