IQNA

Kumbukumbu ya Jinai ya Wazayuni Kuteketeza Moto Msikiti wa al Aqsa

12:44 - August 21, 2018
Habari ID: 3471641
TEHRAN (IQNA)- Siku kama ya leo miaka 49 iliyopita, inayosadifiana na 21 Agosti 1969, Masjidul Aqswa kibla cha kwanza cha Waislamu, kilichomwa moto na Wazayuni.

Katika tukio hilo, eneo hilo takatifu na la kihistoria liliharibiwa vibaya sana. Utawala wa Kizayuni wa Israel ulidai kuwa, kitendo hicho kilifanywa na mtalii wa Kiaustralia. Utawala huo wa Kizayuni ulitayarisha mahakama ya kimaonyesho tu mjini Tel Aviv, na kuchukua uamuzi wa kumuachilia huru mtuhumiwa huyo kwa madai kwamba alikuwa na matatizo ya kiakili. Baada ya kutokea kitendo hicho, nchi za Kiislamu zilikutana na kuamua kuunda Jumuiya ya Nchi za Kiislamu OIC.

Siku ya Kimataifa ya Msikiti

Kwa munasaba wa tukio hilo chungu, Siku ya Kimataifa ya Msikiti huadhimishwa kila mwaka katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na katika baadhi ya nchi duniani ili kukumbuka tukio la kuchomwa moto Msikiti wa al Aqsa huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Mwaka 1969 Mzayuni Michael Dennis Rohan aliuteketeza kwa moto msikiti huo. Wakati huo maafisa wa Israel walitangaza kuwa mtu huyo aliyekuwa na uraia wa Australia, ni Mkisto mwendawazimu, lakini baadaye ilibainika kuwa Dennis Rohan ni Myahudi mwenye misimamo ya kuchupa mipaka na alichoma moto kibla hicho cha kwanza cha Waislamu kwa makusudi. Mbali na hayo ushahidi ulionesha kuwa Wazayuni wengine wenye misimamo mikali walimsaidia Michael Dennis Rohan katika harakati zake za kuchoma msikiti huo.

Jinai za Wazayuni

Quds na maeneo yake matakatifu yamekuwa yakishambuliwa na kuvunjiwa heshima tangu Wazayuni walipovamia na kukalia kwa mabavu ardhi ya Palestina. Katika kipindi chote cha miongo kadhaa iliyopita utawala wa kikatili wa Israel si tu kwamba hauwaonei huruma watoto wadogo na wanawake na umekuwa ukifanya mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu, bali pia umekuwa ukivunja na kuhujumu misikiti na makanisa ya eneo hilo. Pamoja na hayo Msikiti wa al Aqsa ndio unaoshambuliwa na kuvunjiwa heshima zaidi kati ya maeneo yote matakatifu ya Palestina na hilo linafanyika ili kuuharibu kabisa msikiti huo na hatimaye kufuta kabisa utambulisho wa kihistoria wa Palestina. Utawala bandia wa Israel daima umekuwa ukilipa kipaumbele suala la kufuta utambulisho wa Kiislamu wa Quds tukufu na kuharibu maeneo matakatifu na ya kihistoria ya mji huo.Kumbukumbu ya Jinai ya Wazayuni  Kutekteza Moto Msikiti wa al Aqsa

Israel hususan katika miongo miwili iliyopita ya mazungumzo na Wapalestina, imejenga majumba ya kamari, mahoteli, vituo vya anasa na maeneo ya ufuska kandokando ya Msikiti wa al Aqsa kwa shabaha ya kuuzingira msikiti huo. Vilevile utawala huo ghasibu unachimba njia za chini ya msikiti huo kwa lengo la kuuharibu.

Taarifa ya Hamas

Wakati huo huo, harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas, imetangaza kuwa, falsafa ya mapambano na utawala wa Kizayuni wa Israel imejengeka katika msingi wa kufikia lengo la ukombozi wa ardhi za Palestina na kuwatimua Wazayuni maghasibu kutoka ardhi takatifu za Kiislamu na Kikristo hasa mji wa Quds na Msikiti wa Al Aqsa.

Katika taarifa iliyotoelwa kwa munasaba wa kuwadia mwaka wa 49 tokea kuteketezwa moto sehemu ya Msikiti wa Al Aqsa, Hamas imeongeza kuwa: "Makundi yote ya mapambano ya Palestina yana uwezo wa kuendelea na mapambano na muqawama kwa kutumia  njia na suhula zote hadi itakapokombolewa Palestina yote pamoja na mji wa Quds na pia hadi wakimbizi Wapalestina watakapopata haki ya kurejea katika ardhi zao za jadi, kuachiliwa huru wafungwa Wapalestina na kuundwa nchi huru ya Palestina mji mkuu wake ukiwa ni Quds Tukufu (Jerusalem).

3740230

captcha