IQNA

Mgogoro kuhusu Kanisa Katoliki kunyakua Msikiti wa Kihistoria wa Cordoba Uhispania

16:18 - September 17, 2018
Habari ID: 3471677
TEHRAN (IQNA)- Mgogoro kuhusu umiliki wa Msikiti Mkuu wa Crodoba nchini Uhispania unaendelea kutokota baada ya kamati iliyoteuliwa na Baraza la Mji wa Cordoba kupinga hatua ya Kanisa Katoloki kuchukua udhibiti wa msikiti huo.

Msikiti Mkuu wa Cordoba ni wa kihistoria na ulijengwa wakati Uhispania ilipokuwa chinia ya mamlaka ya Waislamu wakati huo ikijulikana kama Andalusia.

Andalusia au Rasi ya Iberia ni ardhi iliyoko kusini magharibi mwa Ulaya ambayo inajumuisha ardhi ya Uhispania, Ureno na eneo la Jabal Twariq au Gibraltar. Nchi hiyo ya Andalusia ilikuwa miongoni mwa maeneo yaliyokuwa na ustaarabu wa Kiislamu kwa kipindi cha miaka 800 na daraja na kiunganishi cha mashariki na magharibi katika masuala mbalimbali ya kisiasa, kiuchumi, kijamii na kiutamaduni.

Kamati iliyoteuliwa na Baraza la Mji wa Cordoba inaongozwa na Federico Mayor Zaragoza, mkurugenzi wa zamani wa UNESCO, ina jukumu la kubaini iwapo jengo la Msikiti Mkuu wa Cordoba, linapaswa kuwa chini ya usimamizi wa umma au kubakia chini usimamizi Kanisa Katoliki. Msikiti huo ulijengwa mwaka 786 Miladia na mtawala Mwislamu wa wakati huo wa Andalusia, Abd al-Rahman I na ulipanuliwa katika miaka iliyofuata na watawala Waislamu. Wakati Wakristo waliporejea katika utawala mwaka 1236 Miladia, msikiti huo ulibadilishwa na kuwa Kanisa Katoliki pamoja na kuwa Waislamu walipinga vikali uamzui huo. Mnamo mwaka 2006, msikiti huo ulibadilishwa rasmi kuwa dayosisi ya Kanisa Katoliki.

Wataalamu wanasema msikiti huo uko katika Orodha ya Turathi za Dunia za Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO na hivyo haupaswi kuwa chini ya kanisa bali unapaswa kusimamiwa na taasisi za umma.

Kamati inayofuatilia suala hiyo imesema kesi ya msikiti huo inapaswa kufikishwa katika Mahakama ya Katiba ya Uhispania ili kubatilisha uamuzi wa kukabidhiwa kanisa usimamizi wa msikiti huo kwani hatua hiyo imetajwa na wengi kuwa ni unyakuzi na ukiukaji sheria za. Mgogoro kuhusu hatima ya msikiti huo ulienea zaidi mwaka 2010 wakati Waislamu walzuiwa kuswali katika eneo hilo lao la ibada.

Majengo makubwa ya Andalusia ni kielelezo cha vipawa na umahiri mkubwa wa Waislamu. Nguzo adhimu za majengo hayo, masakafu, milango na madirisha yenye umbo na sura ya hilali, minara, kuba na nakshi za kuvutia na maridadi na kadhalika ni kielelezo cha usanifu majengo wa Kiislamu wa watu wa Andalusia. Miongoni mwa kazi kubwa zaidi za usanifu majengo wa Kiislamu wa wakati huo ni Msikiti Mkuu wa Córdoba. Msikiti huo ni kati ya misikiti mikubwa zaidi duniani na uko katika eneo la mita mraba 24,000.

Weledi wa historia wanasema ustaarabu na utamaduni huo adhimu wa Kiislamu huko Andalusia ulisambaratika na kuporomoka baada ya miaka 800 kutokana na sababu kadhaa moja ikiwa ni kuenea ufisadi, ufuska wa watawala na kutupiliwa mbali mafundisho asili ya Uislamu.

3466764

captcha