IQNA

Nchi 100 kushiriki katika Kongamano la 32 la Umoja wa Kiislamu nchini Iran

19:56 - November 17, 2018
Habari ID: 3471743
TEHRAN (IQNA) - Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Madehehbu za Kiislamu amesema wanazuoni, wanaharakati wa kisiasa na wasomi kutoka nchi 100 wamealikwa kushiriki katika Kongamano la 32 la Kimataifa la Umoja wa Kiislamu ambalo limepangwa kufanyika mjini Tehran.

Ayatullah Muhsin Araki Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Madhehebu za Kiislamu ameyasema hayo leo katika mkutnao na waandishi wa habari mjini Tehran na kuongeza kuwa: "Pamoja na kuwepo njama za madola ya kiistikbari ya kuvuruga umoja wa madhehebu za Kiislamu, wawakilishi 350 wa nchi 100 watashiriki katika mkutano wa 32 wa Umoja wa Kiislamu mjini Tehran."

Ayatullah Muhsin Araki ameashiria hatua zilizochukuliwa katika kukurubisha madhehbu za Kiislamu katika ulimwengu wa Kiislamu na kusema kumekuwepo na njama za madola ya kibeberu na kiistikbari za kuvuruga umoja wa Kiislamu duniani. Ameendelea kusema kuwa: "Marekani inataka kuibua wimbi la upinzani dhidi ya Iran kwa kutumia vibaraka wake kama vile watawala wa Saudia na utawala wa Kizayuni."

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Madehehbu za Kiislamu  amesema wagone wa kongamano la umoja wa Kiislamu mwaka huu watachunguza njia za kuimarisha umoja na ukuruba wa Waislamu na nchi za Kiislamu katika kukabiliana na maadui.

Kongamano la 32 la Kimataifa la Umoja wa Kiislamu limepangwa kufanyika Novemba 24-26 mjini Tehran.

Mkutano huo hufanyika kila mwaka kwa munasaba wa Wiki ya Umoja wa Kiislamu. Inafaa kuashiria hapa kuwa Wiki ya Umoja wa Kiislamu ni kipindi cha kati ya tarehe 12 na 17 za Mfunguo Sita Rabiu Awwal kipindi ambacho kinasadifiana na kuadhimisha Maulidi na kumbukumbu ya kuzaliwa Bwana Mtume SAW. Kuhusiana na kuzaliwa Bwana Mtume SAW kuna riwaya mbili mashuhuri. Waislamu wengi wa madhehebu ya Kisuni wanaamini kwamba, Bwana Mtume SAW alizaliwa tarehe 12 Mfunguo Sita Rabiul Awwal mwaka wa tembo uliosadifiana na mwaka 570 Miladia.

Kundi jengine la Waislamu ambalo linaundwa zaidi na Waislamu wa madhehebu ya Shiia Ithanaashari linaamini kwamba, Mtume wa Uislamu alizaliwa tarehe 17 Mfunguo Sita Rabiul Awwal mwaka huo huo. Mitazamo hiyo miwili takribani pengo lake ni kipindi cha wiki moja. Kwa kuzingatia hali hiyo, Imam Ruhullah al-Musawi al-Khomeini (MA) Mwasisi na Mwanzilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran akakitaja kipindi hiki cha wiki moja kuwa Wiki ya Umoja, ili Waislamu badala ya kuvutana na kuanza kukuza tofauti za tarehe za kuzaliwa Bwana Mtume SAW wakae pamoja na kujadili umuhimu wa umoja na changamoto mbalimbali zinazowakabili Waislamu na ulimwengu wa Kiislamu kwa ujumla.

3764586

captcha