IQNA

Magaidi wahujumu kwa bomu sherehe za Maulid Afghanistan na kuua watu 53

11:52 - November 21, 2018
Habari ID: 3471747
TEHRAN (IQNA)- Watu wasiopungua 53 wameuawa shahidi katika shambulizi la kigaidi lililolenga mkusanyiko wa Waislamu waliokuwa katika sherehe za Maulidi ya Bwana Mtume Muhammad (SAW) katika mji mkuu wa Afghanistan, Kabul.

Taarifa zinasema , shambulizi hilo lilitokea Juamnne usiku ndani ya Ukumbi wa Uranus mjini Kabul, uliokuwa umekusanya watu zaidi ya elfu moja wakiadhimisha kumbukumbu ya mazazi ya Mtukufu Mtume SAW na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 53.

Duru za habari zinaarifu kuwa, gaidi aliyekuwa amejifunga mabomu aliingia ukumbuni hapo na kujiripua, na kusababisha maafa hayo, huku makumi ya watu wengine wakijeruhiwa.

Hospitali ya Dharura ya Kabul imesema watu 40 wamejeruhiwa vibaya kwenye hujuma hiyo ya kigaidi iliyolenge waumini wa Kiislamu waliokuwa wamekusanyika kwa ajili ya sherehe za Maulid zilizoanza jana Jumanne katika kona mbalimbali za dunia.

Rais Ashraf Ghani ametangaza leo Jumatano kuwa siku ya kitaifa ya kuwaomboleza wahanga wa jinai hiyo ya kigaidi. Ingawaje hakuna kundi lolote lililotangaza kuhusika na shambulizi hilo kufikia sasa, lakini mashambulizi ya kikatili ya aina hii yamekuwa yakifanywa na wanachama wa genge la kigaidi na kitakfiri la Daesh (ISIS). Magaidi wakufurishaji wa ISIS wanafuata pote la Uwahhabi ambalo linapinga vikali Maulid ya Bwana Mtume Muhammad SAW.

/3481683

captcha