Kwa mujibu wa Kituo cha Haki za Binadamu cha Palestina, asilimia 80 ya watoto hao waliuawa katika maandamano ya amani ya Wapalestina katika mpaka wa Ukanda wa Ghaza na ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na Israel. Ripoti hiyo imeongeza kuwa, Jeshi la Israel limewakamata watoto wengine 900 tokea Januari mwaka huu. Ripoti hiyo imesema kuwa wanajeshi wa Israel hukiuka haki za watoto hao waliokamatwa ambao huteshwa vibaya.
Tangu mwanzoni mwa mwaka huu wa 2018, Wapalestina zaidi ya 310 wameuawa kwa kupigwa risasi na wanajeshi wa utawala haramu wa Israel na aghalabu ya waliouawa walikuwa ni raia ambao hawakuwa na silaha.
Mwezi Okotoba, Harakati ya Kupigania Ukombozi wa Palestina, PLO, ilisema jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel limekuwa likiwaua kwa makusudi watoto wa Palestina. Mwanachama wa Kamati ya Utendaji ya PLO, Bi. Hannan Ashrawi anasema vitendo hivyo vya Israel ni ukiukwaji wa wazi wa sheria na kanuni za kimataifa.
Ripoti iliyochapishwa Juni mwaka jana ilibaini kuwa Jeshi la Utawala haramu wa Israel limeua shahidi watoto zaidi ya 3,000 Wapalestina tangu ulipoanza mwamako wa pili wa Wapalestina maarufu kama Intifadha mwezi Septemba 2000.
Hii ni katika hali ambayo ripoti tofauti za kimataifa zinasema kwamba watu wa matabaka tofauti ya Palestina wakiwemo watoto, wanakabiliwa na jinai na vitendo vya mabavu na mateso vya utawala wa Kizayuni ambao hautambui mipaka yoyote ya sheria. Ukiukaji wa haki za watoto wa Palestina unaofanywa na utawala wa Israel hauna mwisho na utawala huo unadumisha jinai hizo dhidi ya watoto hao bila ya kuwa na hofu yoyote ya kufikishwa mbele ya vyombo vya mahakama wala kuwajibishwa na jamii ya kimataifa.