IQNA

Mkuu wa zamani wa kitivo cha Qurani mjini Madina afariki gerezani Saudia

14:19 - January 21, 2019
Habari ID: 3471813
TEHRAN (IQNA)-Mhubiri mashuhuri Saudi Arabia, Ahmed al-Amari, amefariki mjini Jeddah, Saudi Arabia.

Kwa mujibu wa ujumbe wa Twitter uliosambazwa katika akaunti ya 'Wafungwa wa Kiitikadi Saudia' imesema Sheikh al-Amari, ambaye aliwahi kuwa mkuu wa Kitivo cha Qur'ani katika Chuo Kikuu cha Madina, alifariki dunia Jumapili Januari 20.

Al-Amari alikamatwa na kufungwa jela Agosti mwaka 2018 baada ya kuchapisha kitabu kilichokuwa na ushauri kwa watawala wa Saudia. Mnamo Januari 13 kulienea ripoti kuwa alikuwa amepooza ubongo baada ya kudungwa sindano ya sumu akiwa gerezani kufuatia amri ya watawala wa Saudia.  Mwanazuoni huo alifariki dunia akiwa anapata matibabu hospitalini mjini Jeddah.

Hivi karibuni pia kulikuwa na ripoti kuwa, mwanaharakati wa kisiasa nchini humo, Yaser al-Ayyaf yuko katika hali mbaya ya kiafya kutokana na majeraha ya kuteswa na kuchomwa moto alipokuwa akizuiliwa na vyombo vya usalama vya Saudia.

Mwenendo huo wa kuwanyanyasa, kuwafunga jela na hata kuwaua wanazuoni na wasomi wa Kiislamu nchini Saudi Arabia ulianza kushika kasi baada ya utawala wa kifalme wa nchi hiyo kumfunga jela na hatimaye kumuua mwanachuoni na mtetezi mkubwa wa haki za binadamu wa nchi hiyo Ayatullah Nimr Baqir Nimr mwaka 2016.

Mwishoni mwa mwaka uliomalizika, Jumuiya ya Kimataifa ya Wanazuoni wa Kiislamu ilitoa taarifa ya kulaani mwenendo huo wa kubinywa wanazuoni wakosoaji utawala wa kiimla Saudia.

3783082

captcha