IQNA

China inatumia kamera maalumu kuwachunguza Waislamu

14:01 - February 21, 2019
Habari ID: 3471848
TEHRAN (IQNA) –Serikali ya China inaendeleza ukandamizaji wake wa jamii ya Waislamu nchini humo na sasa inatumia kamera maalumu kwa lengo la kuwachunguza na kuwadhibiti Waislamu.

Taarifa zinasema kuna shirika moja la China ambalo limepewa kazi maalumu ya kuwachunguza Waislamu wapatao milioni 2.5 katika eneo ambalo serikali ya Beijing imekithirisha ukandamizaji Waislamu.

Imebainika kuwa kamera maalumu zimewekwa katika miji ya eneo la Xinjiang na kwamba mradi huo unasimamiwa na shirika la SenseNets Technology.

Wataalamu wanasema mradi huo ni maalumu kwa ajili ya kuwapelekeza Waislamu wa jamii wa Uygur na umefadhiliwa na wakuu wa mkoa wa Xinjiang.

Kwa mujibu wa Victor Gevers, mtaalamu wa usalama wa mitandaoni kutoka Uholanzi, uchunguzi umebaini kuwa mradi huo umeanzishwa ili kuwadhibiti Waislamu. Amesema uchunguzi wake umebaini kuwa kila harakati ya Waislamu milioni 2.5 katika eneo hilo inafuatiliwa. Amesema kamera hizo kwa mfano zinaweka rekodi za msikiti alikofika Mwislamu pamoja na migahawa pamoja na maeneo mengine.

Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Kuangamiza Ubaguzi wa Rangi imesema imeandika ripoti kuhusu masaibu ambayo Waislamu wanakumbana nayo katika kambi hizo.

Uislamu ni kati ya dini tano ambazo zinatambuliwa rasmi na Chama cha Kikomunisti China ambapo kuna takribani Waislamu milioni 23 nchini humo.

Katika miaka ya hivi karibuni kumeongezeka sera za kuwakandamiza Waislamu katika nchi hiyo hasa katika jimbo la Xinjiang wenye Waislamu Zaidi ya milioni 10 kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi na misimamo mikali.

3792068

captcha