IQNA

Mpango wa Adhana ya Pamoja katika Misikiti ya Cairo, Misri

9:54 - March 02, 2019
Habari ID: 3471858
TEHRAN (IQNA) – Serikali ya Misri inatekeleza mpango wa majaribio wa adhana ya pamoja katika misikiti 113 nchini Cairo ili kuzuia sauti mbali mbali katika vipaza sauti vya misikiti wakati wa adhana.

Kwa mujibu wa mpango huo, katika wakati wa Sala kutakuwa na adhana moja itakayopokewa kupitia Radio ya kitaifa ambapo misikiti yote itatakiwa kuunganisha vipaza sauti na radio ili kurusha hewani adhana.

Wizara ya Wakfu ya Misri inasimamia mradi huo wa majaribio katika misikiti 113 na baada ya kumalizika itatoa ripoti ya kiufundi. Wafanyakazi wa misikiti watafundishwa namna ya kuwasha mikrofoni wakati wa adhana na kuzinuganisha na radio. Wizara hiyo imesema  Waadhini katika mradi huo wamechaguliwa baada ya sauti zao kuchunguzwa kwa kina.

Hatahivyo mradi huo umepingwa na baadhi ambao wanalalamika kuwa misikiti haipaswi kualzimishwa kutumia Adhana ya radio. Aidha baadhi wana wasiwasi kuwa mpango huo wa Wizara ya Wakfu Misri utadhoofisha hadhi ya Adhana na Muadhini katika Uislamu.    

Waziri wa zamani wa Wakfu nchini Misri Mahmoud Zaqzouq mwaka 2014 alitetea pendekezo la Adhana moja kwa kusema kuwa sauti moja ya Adhana  katika misikiti yote ni kwa maslahi ya watu wote.

Sheria ya Adhana moja ilitangazwa kwa mara ya kwanza Misri mwaka 2010 kwa lengo la kuleta nidhamu katika adhana ya misikiti zaidi ya 4,000 kote Cairo. Baadhi walisema ni kero wakati wa sala kusikia kila msikiti ukiwa na adhana ya aina yake na hivyo walitaka kuwepo sauti moja ya adhana katika misikiti yote.

Utekelezwaji wa sheria hiyo ulisitishwa mwaka 2011 baada ya kuibuka mapinduzi ya wananchi yaliyopelekea utawala uliokuwepo kuangushwa.

3468028

captcha