IQNA

Erdogan: Jumba la Makumbusho la Hagia Sofia mjini Istanbul litageuzwa kuwa msikiti

23:20 - March 29, 2019
Habari ID: 3471893
TEHRAN (IQNA)- Jumba la Makumbusho la Hagia Sophia mjini Istanbul litageuzwa na kurejea katika hadhi yake ya msikiti, ameamuru Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki.

"Hagia Sophia halitakuwa tena jumba la makumbusho. Hadhi yake itabadilika na litakuwa msikiti," alisema Erdogan siku ya Jumatano.

"Watalii wanokuja kutembelea misikiti Istanbul sasa watatembelea Msikiti wa Hagia Sophia," alisisitiza rais wa Uturuki.

Erdogan amepuuzilia mbali maafisa wa nchi za kigeni ambao wamekosoa uamuzi wake huo na kusema wamekuwa wakinyamaza kimya wakati Msikiti wa Al Aqsa unapovunjiwa heshima katika mji wa Quds (Jerusalem). "Wale wanaonyamaza kimya wakati Msikiti wa Al Aqsa unapohujumiwa na kuvunjiwa heshima hawawezi kutuambia cha kufanya kuhusu hadhi ya Hagia Sophia," amesema Rais wa Uturuki.

Jengo la Hagia Sophia ambalo baadhi ya wanahistoria wamelitaja kuwa miongoni mwa maajabu ya dunia  ni kati ya maeneo yanayotembelewa zaidi duniani kutokana na vivutio vyake vya sanaa na usanifu majengo.

Jengo hilo lilijengwa mwaka 537 Miladia (CE) na lilipata umaarufu kutokana na kuba lake adhimu na wakati huo lilikuwa jengo kubwa zaidi duniani. Tokea mwaka 537 hadi 1453 lilikuwa ni Kanisa la Mashariki la Kiothodoxi na makao makuu ya Kasisi Mkuu wa Constantinople. Kwa muda mfupi, kati yaani kati ya mwaka 1204 hadi 1261, jengo hilo liligeuzwa na Wapiganaji wa Nne wa Msalaba kuwa Kanisa Katoliki. Wakati watawala wa silsila ya  Wauthmaniya (Ottomans) walipouteka mji huo, mnamo mwaka 1453 Fatih Sultan Mehmet aliagiza jengo la Hagia Sophia litumike kama msikiti. Hadhi hiyo ya Hagia Sophia kama msikiti iliendelea kwa muda wa miaka 482 hadi mwaka 1935 wakati muasisi wa Jamhuri ya Uturuki, Mustafa Kemal Ataturk alipoagiza ligeuzwe na kuwa jengo la makumbusho.

Erdogan: Jumba la Makumbusho la Hagia Sofia mjini Istanbul litageuzwa kuwa msikiti

Jengo hilo lilikarabatiwa wakati wa Wauthmaniya na minara ikaongezwa na hivyo kulifanya kuwa moja kati ya nembo muhimu zaidi za usanifu majengo duniani. Sasa kwa dikrii ya Rais Erdogan, jengo hilo litarejea katika hadhi yake ya msikiti.

3468197

captcha