IQNA

Ripoti: China inabomoa misikiti muhimu eneo la Xinjiang

10:05 - April 10, 2019
Habari ID: 3471908
TEHRAN (IQNA) - Picha za satalaiti zinaonyesha kuwa serikali ya China inabomoa misikiti muhimu ya eneo lenye Waislamu wengi la Xinjiang.

Wanaharakati wanasema picha za satalaiti za kabla na baada zinaonyesha kuw akwa uchache misikiti miwili muhimu na mikubwa imebomolewa katika eneo la Xinjiang. Kati ya misikiti iliyobomolewa ni Msikiti wa Keriya Aitika (kwenye picha) uliojengwa miaka 800 iliyopita na ambao uliwekwa katika Turathi za Usanifu Majengo China mwaka 2017. Ripoti pia zinasema utawala wa China umebomoa Msikiti wa Kargilik katika eneo hilo.

Mwezi Septemba mwaka jana, Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Human Rights Watch limeituhumu serikali ya China kuwa inatekeleza kampeni ya makusudi ya kukiuka haki za Waislamu wa Jamii ya Uighur eneo la Xinjiang.

Ripoti hiyo yenye kurasa 117 inaituhumu serikali ya China kuwa inawakamata kiholela Waislamu na kuwatesa vibaya wakiwa korokoroni.

Kwa mujibu wa wataalamu wa haki za binadamu katika Umoja wa Mataifa, Waislamu takribani milioni moja wa jamii ya Uighur wanashikiliwa katika kambi za kuwafunza Usosholisti wa Kichina na wanalazimishwa kwa kisingizio cha kukabiliana na ugaidi.

Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Kuangamiza Ubaguzi wa Rangi imesema imeandika ripoti kuhusu masaibu ambayo Waislamu wanakumbana nayo katika kambi hizo.

Uislamu ni kati ya dini tano ambazo zinatambuliwa rasmi na Chama cha Kikomunisti China ambapo kuna takribani Waislamu milioni 23 nchini humo.

Katika miaka ya hivi karibuni kumeongezeka sera za kuwakandamiza Waislamu katika nchi hiyo hasa katika jimbo la Xinjiang lenye Waislamu Zaidi ya milioni 10 kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi na misimamo mikali.

/3468258

 

 

captcha